IQNA

Iran inaunga mkono mpango wowote wenye kuhitimisha uvamizi dhidi ya Yemen

22:35 - March 23, 2021
Habari ID: 3473756
TEHRAN (IQNA)- Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetangaza kuwa Iran inaunga mkono mpango wowote wa kuleta amani Yemen.

Katika taarifa wakati huu wa kuwadia mwaka wa saba tokea muungano wa kijeshi wa Saudia uanzishe hujuma dhidi ya Yemen,  Wizara ya Mambo ya Iran imetangaza kuwa Tehran inaunga mkono, mpango wowote ambao utahitimisha hujuma dhidi ya Yemen sambamba na usitishwaji vita kote katika nchi hiyo na pia kuhitimisha ukaliwaji mabavu, kuondolewa mzingiro wa kiuchumi, kuanza mazungumzo ya kisiasa na hatimaye kuachiwa Wayemen waainishe mustakabali wao wa kisiasa.

Hali kadhalika taarifa hiyo imetangaza kuwa, Iran inachukizwa na kuendelea jinai dhidi ya watu wa Yemen wasio na hatia.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran katika taarifa hiyo imesema mzingiro wa kiuchumi na kijeshi umewalenga watu milioni 24 wa Yemen na kila siku makumi ya watu hupoteza maisha kutokana na kudondoshewa mabomu au njaa, magonjwa, ukosefu wa chakula, dawa na mafuta katika vituo vya afya.

Taarifa hiyo imesema kwa mujibu wa takwimu za kimataifa, na hata baadhi wa waungaji mkono wa Saudia kijeshi na kisiasa wamekiri kuwa, vita vya Saudia dhidi ya Yemen vimeambatana na jinai ambazo zinaweza kufuatiliwa kimataifa na hivyo ni jukumu la asasi za kimataifa na watetezi wote wa haki za binadamu kufuatilia kisheria jinai hizo katika uga wa kimataifa.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesisitiza kuwa waungaji mkono wa muungano vamizi wa Saudia wanadai kuwa wanasitisha uungaji mkono huo lakini pamoja na hayo wanaendelea kuuzia muungano huo silaha na hata kuupa usaidizi kiufundi na pia wataalamu wa kijeshi wa nchi hizo wanatoa huduma za moja kwa moja kwa Saudia na kwa msingi huo ni washirika wa jinia dhidi ya watu wa Yemen.

Siku ya Jumatu, Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudia Mwanamfalme Faisal bin Farhan Aal Saud aliwasilisha kile alichodai kuwa ni ‘pendekezo la amani’ la kumaliza mapigano Yemen. Pendekezo hilo linajumuisha kufunguliwa uwanja wa ndege wa Sana’a na kuruhusua chakula na mafuta kuingia Yemen kupitia bandari ya Hudaydah. Maeneo hayo mawili yanadhibitiwa na Harakati ya Ansarullah.

Hatahivyo, Mwanachama mwandamizi wa Baraza Kuu la Kisiasa Yemen ametupilia mbali kile ambacho Saudia imedai eti ni ‘pendekezo la amani’ na kusema kile ambacho taifa la Yemen linataka ni muungano wa kivita unaoongozwa na Saudia usitishe vita kilamilifu na uondoe mzingiro dhidi ya nchi hiyo.

 

Katika ujumbe kupitia ukurasa wake wa Twitter Mohammed Ali al-Houthi ameandika: “Tulikuwa tunataraji kuwa Marekani na Saudia zingetangaza usitishwaji vita wa muda na kuwasilisha pendekezo la kuondoa mzingiro. Wanapaswa kuonyesha wanalipa suala hili uzito kwa kuruhusu meli kutia nanga katika bandari ya Hudaydah.”

 

Utawala dhalimu wa Saudia ulianzisha mashambulizi dhidi ya Yemen mnamo Machi 2015 kwa lengo la kuiondoa madarakani Harakati ya Ansarullah na kumrejesha madarakani kibaraka wake, Abdrabbuh Mansour Hadi, rais wa zamani wa nchi hiyo aliyejiuzulu na kukimbilia Riyadh. Hata hivyo hadi sasa Saudia na washirika wake wameshindwa kufikia malengo yao kutokana na kusimama kidete wananchi wa Yemen wakiongozwa na Harakati ya Ansarullah. Harakati hiyo imekuwa ikitekeleza mashambulizi ya kulipiza kisasi ndani ya ardhi ya Saudi Arabia ambapo imelenga mara kadhaa vituo vya kusafisha mafuta na pia viwanja vya ndege vinavyotumiwa na jeshi vamizi la utawala huo wa kifalme.

Hivi karibuni, Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) lilisema kati ya Januari na Juni 2021, asilimia 54 ya Wayemen, yaani watu milioni 16.2, watakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula kutokana na vita vya Saudia dhidi ya nchi hiyo.

Aidha mwezi Disemba mwaka jana,  Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) ilitangaza kuwa vita vya Saudi Arabia dhidi ya Yemen vimepelekea zaidi ya watu 233,000 kupoteza maisha katika kipindi cha miaka sita iliyopita.

3960990

captcha