IQNA

Kiongozi wa Ansarullah

Saudia imebomoa misikiti 1400 katika vita dhidi ya Yemen

11:31 - March 26, 2021
Habari ID: 3473762
TEHRAN (IQNA) - Kiongozi wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen amesema muungano vamizi wa kijeshi umebomoa misikiti 1400 katika mashambulizi yake maeneo mbali mbali nchini Yemen.

Akizungumza kwa njia ya televisheni ya Al Masirah ya Yemen Alhamisi, wakati huu vita dhidi ya Yemen vinaingia mwaka wa saba, Kiongozi wa Harakati ya Ansarullah Sayyed Abdul-Malik Badruddin Al-Houthi amewapongeza watu wa Yemen kwa kusimama kidete kukabiliana na maadui wavamizi.

Aidha amesema Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu ziliishambulia Yemen katika fremu ya kutekeleza njama za Marekani na Utawala wa Kizayuni wa Israel katika eneo la Asia Magharibi (Mashariki ya Kati).

Amesema Saudia na waitifaki wake katika eneo hawakuwa na msingi wowote wa kisheria katika kuanzisha vita dhidi ya Yemen mnamo Machi 25 mwaka 2015.  Amesema ukweli kuwa balozi wa Saudia wakati huo nchini Marekani, Adel al-Jubeir, ndiye aliyetangaza kuanza hujuma dhidi ya Yemen ni dalili ya wazi kuhusu nani hasa aliyeamurisha vita hivyo vianze.  Aidha Sayyed Abdul-Malik Badruddin Al-Houthi amesema kabla ya Saudia kuanzisha vita dhidi ya Yemen, kwa miezi kadhaa utawala wa Kizayuni wa Israel ulikuwa ukichochea vita hivyo.

Kiongozi wa Ansarullah pia ametupilia mbali pendekezo eti la amani la Saudi Arabia na kusema ni vipi wale walioanzisha vita dhidi ya Yemen sasa wanadai kuwa wanahamu ya kuwa wapatanishi wa amani?

Ameongeza kuwa, wanajeshi vamizi wanaoongozwa na Saudia wameuaa maelfu ya Wayemen mbali na kudondosha mabomu misikitini, taasisi za kielimu na maeneo mengine ya mijimuiko. Aidha amesema madakati wengi na wafanyakazi wa sekta ya afya wameuawa baada muungano huo wa Saudia kuvamia vituo vya afya. Kiongozi wa Ansarullah amesema majeshi vamizi ya Saudia yamekuwa pia yakilenga ameneo yenye kutoa huduma muhimu za umma kama vile maji na umeme.  Halikadhalika ametabiri kuwa Saudia na waitifaki wake watatumbukia zaidi katika kinamasi nchini Yemen iwapo vita vitaendelea.

Mwezi Machi 2015, Saudi Arabia ikiungwa mkono na Marekani, Imarati na nchi zingine kadhaa iliivamia kijeshi Yemen na kuiwekea mzingiro nchi hiyo wa nchi kavu, baharini na angani ambao unaendelea hadi sasa.

Wizara ya Haki za Binadamu ya Yemen imetangaza kuwa raia 43,582 wameuliwa moja kwa moja na majeshi ya muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia tangu muungano huo ulipoanzisha hujuma za kijeshi dhidi ya nchi hiyo.

Ripoti iliyotolewa Alkhamisi na wizara hiyo imeeleza kuwa, maelfu ya mashambulio ya kijeshi yaliyofanywa na muungano vamizi wa kijeshi wa Saudia yamesababisha vifo vya watu 43,582 wakiwemo watoto 7,999 na wanawake 5,184. Idadi ya waliopoteza maisha kwa njia isiyo ya moja kwa moja kutokana na vita hivyo ni kubwa zaidi. Kwa mujibu  Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) ilitangaza kuwa vita vya Saudi Arabia dhidi ya Yemen vimepelekea zaidi ya watu 233,000 kupoteza maisha katika kipindi cha miaka sita iliyopita.

Hivi karibuni, Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) lilisema kati ya Januari na Juni 2021, asilimia 54 ya Wayemen, yaani watu milioni 16.2, watakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula kutokana na vita vya Saudia dhidi ya nchi hiyo.

/3961183

captcha