IQNA

Ansarullah: Pendekezo la amani la Saudia halina jipya

18:41 - March 24, 2021
Habari ID: 3473757
TEHRAN (IQNA)- Mohammed Abdul Salam, msemaji wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen amesema pendekezo la amani la Saudia ‘halina jipya’ kwani halijumuishi takwa la Ansarullah la kuondolewa mzingiro kikamilifu dhidi ya Yemen hasa katika uwanja wa ndege wa Sana’a na bandari ya Hudaydah.

“Tulitaraji Saudia ingetangaza kusitisha kikamilifu mzingiro wa viwanja vya ndege na bandari na kuruhusu meli 14 ambazo zimezuiwa na muungano huo kutia nanga bandarini,” amesema

Aidha amebaini kuwa Ansarullah itaendelea kushiriki katika mazungumzo ya ya kusaka amani Yemen.

Siku ya Jumatu, Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudia Mwanamfalme Faisal bin Farhan Aal Saud aliwasilisha kile alichodai kuwa ni ‘pendekezo la amani’ la kumaliza mapigano Yemen. Pendekezo hilo linajumuisha kufunguliwa uwanja wa ndege wa Sana’a na kuruhusua chakula na mafuta kuingia Yemen kupitia bandari ya Hudaydah. Maeneo hayo mawili yanadhibitiwa na Harakati ya Ansarullah.

Aidha waziri huyo amesema mazungumzo ya kisiasa baina ya wawakilishi wa serikali iliyopinduliwa ya Abd Rabbuh Mansour Hadi inayopata himaya ya Saudia na Harakati ya Ansarullah yataanza.

Naye Mwanachama mwandamizi wa Baraza Kuu la Kisiasa Yemen ametupilia mbali kile ambacho Saudia imedai eti ni ‘pendekezo la amani’ na kusema kile ambacho taifa la Yemen linataka ni muungano wa kivita unaoongozwa na Saudia usitishe vita kilamilifu na uondoe mzingiro dhidi ya nchi hiyo.

Katika ujumbe kupitia ukurasa wake wa Twitter Mohammed Ali al-Houthi ameandika: “Tulikuwa tunataraji kuwa Marekani na Saudia zingetangaza usitishwaji vita wa muda na kuwasilisha pendekezo la kuondoa mzingiro. Wanapaswa kuonyesha wanalipa suala hili uzito kwa kuruhusu meli kutia nanga katika bandari ya Hudaydah.”

Aidha ameitaka Marekani na muungano vamizi wa Saudia ambao unaendeesha vita dhidi ya Yemen kuafiki ubunifu wa  Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen wenye lengo la kurejesha amani kamili nchini humo.

Naye Mohammed al Bukhaiti, mwanachama wa Baraza Kuu la Kisiasa Yemen amesema Majeshi ya Yemen na waitifaki wao wataendelea kutekeleza mashambulio ya ulipazaji kisasi ndani ya Saudia hadi amani ya kudumu ipatikane. Ameongeza kuwa, amani haiwezi kupatikana Yemen kwa tangazo la upande mmoja la usitishaji vita. Amesema muungano vamizi  wa Saudia ukishirikana na mamluki wake ungali unaendeleza  vita na hiyo ni dalili ya kutokuwa na azma imara ya kurejesha amani Yemen.

Wakati huo huo masaa kadhaa baada ya Saudia kutangaza usitishwaji vita ndege zake za kivita zimedondosha mabomu katika maeneo kadhaa ya kiraia kote Yemen mapema Jumanne. Ndege hizo zimedondosha mabomu katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Sana’a na maeneo ya raia katika wilaya ya Sirwah katika mkoa wa Ma’rib na pia wilaya ya Abs mkoani Hajjah.

3961093

Kishikizo: yemen ansarullah saudia
captcha