IQNA

Familia ya kijana shujaa Muirani yapata zawadi ya Qur’ani Tukufu kutoka Kiongozi Muadhamu

13:55 - October 03, 2021
Habari ID: 3474374
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ameitunuku familia ya shujaa shahidi Landi zawadi ya Qur’ani Tukufu kutokana na kitendo cha kishujaa cha kijana huyo cha kuokoa maisha ya wanawake wawili hivi karibuni.

Mshahafu huo umekabidhiwa familia ya  Shahidi Ali Landi na Dkt. Payman Jebeli Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (IRIB) wakati alipoitembelea familia hiyo jana katika mkoa wa Khuzestan kusini mwa Iran.

Katika ujumbe aliouandika katika Msahafu huo, Ayatullah Khamenei amesema: “Zawadi hii ni kwa ajili ya familia azizi na yenye subira ya kijana shujaa mwenye kujitolea, Ali Landi, ambaye aliweza kuonyesha taswira ya kuwa kigezo kwa kizazi cha vijana. Mwenyezi Mungu Amrehemu na awabariki wazazi na familia yake.”

Landi aliaga dunia Septemba 24 kutokana na majeraha ya moto aliyopata.

Barobaro huyo shujaa aliyekuwa na umri wa miaka 15 hivi karibuni alikimbia na kufika katika nyumba ya jirani ambayo ilikuwa ikiteketea moto huku kukuwa na wanawake wawili ndani ambao walikuwa wameshindwa kutoka katika nyumba hiyo iliyo mjini Izeh mkoani Khuzestan. Alifanikiwa kuwanusuru wanawake hao aktika tukio hilo la Septemba  lakini alipata majeraha. Shujaa Ali alilazwa katika Hospitali ya Taleqani mjini Ahvaz huku asilimia 90 ya mwili wake ukiwa na majeraha ya moto na baada ya hapo alipoteza maisha. Mnamo Septemba 25 Ayatullah Khamenei aliafiki pendekezo ya Shirika la Mashahidi na Masuala ya Maveterani kuwa shujaa Landi atangazwe kuwa shahidi.

3475879/

captcha