
Katika ujumbe wake wa Alhamisi, rais wa Iran amesisitiza kuhusu sifa za kiroho za Nabii Isa hasa uhuru, uadilifu na huruma, ambazo pia zimetajwa katika Qur’ani Tukufu, akizieleza kuwa ni mifano ya milele kwa wanadamu wote.
Hapa chini ni matini kamili ya ujumbe huo.
Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu
Mheshimiwa Papa Leo wa Kumi na Nne, Kiongozi wa Wakatoliki duniani,
Kwa dhati kabisa nakuletea pongezi kufuatia kuwadia maadhimisho ya kuzaliwa kwa Nabii Isa bin Maryam (amani iwe juu yake) pamoja na kuanza kwa mwaka mpya wa 2026.
Kuzaliwa kwa Nabii Isa Masihi (amani iwe juu yake) kunatukumbusha sifa zake za kiroho: uhuru wa nafsi, kupinga dhulma, na upendo kwa viumbe, ambazo pia zimeenziwa ndani ya Qur’ani Tukufu. Tunatarajia kwamba kwa kufuata amri za Mwenyezi Mungu na mafundisho ya Mitume, ulimwengu utashuhudia kutimia kwa uadilifu, amani na uhuru kwa wote.
Katika zama hizi ambapo uhalifu wa madola makubwa, kwa sababu ya nguvu zao zisizo na mipaka, unaisukuma jamii ya kimataifa kuelekea vita na maangamizi, suluhisho la matatizo ya binadamu linahitaji hekima ya pamoja, mtazamo mpya, tafakuri na mazingatio. Kwa hivyo, kupitia juhudi za viongozi na wasomi wasiofungamana na wavamizi wa nyanja za ushawishi na utajiri, tunaweza kufungua njia mpya ya kutimiza amani, usalama na uhuru kwa mataifa yote yaliyodhulumiwa na kuonewa.
Naomba kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu akupe afya na mafanikio, awabariki wafuasi wa Nabii Isa (amani iwe juu yake), na alete amani na utulivu kote duniani.
Masoud Pezeshkian
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran
4324974