
Harakati ya Kiislamu ya Kupigania Ukombozi wa Palestina, Hamas, imelaani kwa nguvu kitendo cha Israel cha kufuata ajenda hatari ya ‘Kuyahudisha’ Ukingo wa Magharibi uliokaliwa kwa mabavu, baada ya utawala huo kuinyang’anya manispaa ya al-Khalil mamlaka ya usimamizi na ujenzi katika msikiti huo wa Kihisotria. Katika tamko lake, Hamas imesema: ‘Utawala wa Kizayuni unataka kudhoofisha utambulisho wa msikiti, pamoja na utambulisho wa Kiarabu na Kiislamu wa al-Khalil.’
Tamko hilo limetolewa baada ya jeshi la Israel kuchukua mamlaka ya manispaa juu ya Msikiti wa Ibrahimi kutoka kwa Wapalestina, hatua hiyo iliyochukuliwa Jumatano itadhoofisha usimamizi wa Kiislamu wa eneo hilo. Hamas imeongeza kuwa: ‘Hii ni sehemu ya juhudi pana za Israel za kutwaa ardhi na maeneo matakatifu ya Wapalestina.’
Hamas pia ilibainisha kuwa hatua za Israel zinakiuka uamuzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Utamaduni, UNESCO, wa kuorodhesha Msikiti wa Ibrahimi na Mji wa Kale wa al-Khalil kama sehemu ya urithi wa dunia ulio hatarini. Katika sehemu nyingine ya tamko, Hamas imetoa wito kwa jumuiya ya kimataifa hasa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC), Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, taasisi za kisheria na mashirika yanayohusiana na Umoja wa Mataifa — hususan UNESCO — kuchukua hatua za haraka kukabiliana na udhibiti hatari wa Israel juu ya maeneo matakatifu ya Kiislamu na Kikristo katika ardhi zilizokaliwa.
Manispaa ya al-Khalil pia imelaani uamuzi wa Israel, ikisema ni ‘ukiukaji mkubwa na usio halali’ na sehemu ya mashambulizi ya kimfumo dhidi ya hali ya sasa ya msikiti na mamlaka ya Wapalestina waliokabidhiwa jukumu la kusimamia.
Mnamo mwaka 1994, mkazi wa Kizayuni aliyekuwa na silaha aliingia msikitini katika mwezi mtukufu wa Ramadhani na kufyatua risasi kwa waumini wa Kiislamu, na kuua watu 29 na kuwajeruhi zaidi ya 120. Baada ya mauaji hayo, usimamizi wa eneo uligawanywa kati ya Wapalestina na Waisraeli chini ya makubaliano ya mwaka 1997.
Kwa mujibu wa makubaliano hayo, Waqf wa Kiislamu pamoja na Manispaa ya al-Khalil walikuwa na jukumu la kusimamia msikiti, ikiwemo ujenzi na ukarabati. Lakini hatua ya hivi karibuni ya Israel imewanyang’anya mamlaka haya, na kuzua hofu kuwa Israel inakaribia kutwaa udhibiti kamili.
3495931