IQNA

Sisistizo la UN kuwa hatua za utawa Kizayuni wa Israel huko Golan ni batili

23:47 - December 10, 2021
Habari ID: 3474660
TEHRAN (IQNA)- Umoja wa Mataifa mapema leo Ijumaa umepasisha azimio linalolaani na kubatilisha hatua zote za Israel katika eneo la Syria la Golan linalokaliwa kwa mabavu na utawala huo na kuutaka utawala wa Kizayuni ukomeshe hatua zote zinazokiuka sheria za kimataifa.

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limesisitiza kuwa, hatua zilizochukuliwa na zitakazochukuliwa na utawala ghasibu wa Israel kwa ajili ya kubadili utambulisho na hali ya kisheria ya eneo la Golan la Syria ni batili na zinakiuka kanuni na sheria za kimataifa. 

Nchi 149 zimelipigia kura ya ndiyo azimio hilo lililopewa jina la "Golan inayokaliwa kwa mabavu" ambalo limepingwa na Marekani na utawala haramu wa Israel.

Azimio hilo limeitaka Israel, ambayo ni utawala vamizi na ghasibu, kutekeleza maamuzi yanayohusiana na eneo linalokaliwa kwa mabavu la Golan hususan azimio nambari 497 la Baraza la Usalama lililopasishwa mwaka 1981 ambalo linasisitiza kuwa maamuzi ya utawala huo ya kulazimisha kanuni na sheria zake eneo la Golan la Syria linalokaliwa kwa mabavu ni batili na hayana taathira za sheria. 

Azimio hilo pia limeitaka Israel kufuta mara moja maamuzi yake na kukomesha mipango yake ya kubadili sura ya mji, muundo wa jamii na hali ya kisheria ya eneo la Golan la Syria lililovamiwa na kukaliwa kwa mabavu hususan ujenzi wa vitongoji vya walowezi katika eneo hilo.

Hili ni azimio la pili la Umoja wa Mataifa katika mwezi huu wa Disemba linalolaani hatua za utawala wa Kizayuni wa Israel huko Golan. Siku chache zilizopita pia Umoja wa Mataifa ulipasisha azimio lililoitaka Israel kuondoka kikamilifu eneo la Golan la Syria na kurejea katika mpaka wa tarehe 4 Juni mwaka 1967. 

2623225

captcha