IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Taifa la Iran limegeuza kuuawa shahidi Jenerali Soleimani kuwa ni fursa

15:13 - January 09, 2022
Habari ID: 3474784
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyed Ali Khamenei amesema maadui walidhani kuuawa shahidi kamanda shujaa katika vita dhidi ya ugaidi Luteni Jenerali Qassem Soleimaini kungekuwa tishio kwa Iran lakini watu wa Iran wamegeuza tukio hilo kuwa fursa kutokana na imani yao ya kidini.

Kiongozi Muadhamu ameyasema hayo katika hotuba aliyotoa leo kwa mnasaba wa mwamko wa wananchi wa  Januari 9, 1978 katika mji mtakatifu wa Qum dhidi ya utawala wa zamani wa Shah Pahlavi ambao ulikuwa unapata himaya ya Marekani.

Kiongozi Muadhamu ameongeza kuwa: "Mahesabu mabovu ya Marekani yangali yanaendelea na mfano wa hilo ni kuuawa shahidi Shahidi Soleimani."

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, mazishi ya kihistoria ya Shahidi Qasem Soleimani ni kielelezo cha mlipuko wa hamasa inayotengeneza fursa ya wananchi na kubainisha kuwa: Katika shughuli hiyo, taifa la Iran kwa mara nyingine tena lilionesha waziwazi umoja na utambulisho wake wa kidini na kimapinduzi; na lau mwili huo mtukufu ungepelekwa Syria, Lebanon na Pakistan ungepewa mapokezi makubwa ya mataifa ya Waislamu kama ilivyokuwa nchini Iran na huko Iraq.

Ayatullah Khamenei amekitaja kitendo cha kumuua shahidi Kamanda Soleimani kuwa ni mfano wa kuendelea mahesabu mabovu ya Wamarekani na kuongeza kuwa: Magaidi walitaka kumuua Kamanda Soleimani aliyekuwa nembo ya harakati adhimu aliyoiwakilisha, lakini harakati kubwa ya taifa la Iran na watu wa mataifa mengine ya kuonesha mapenzi na uungaji mkono wao kwa jamadari huyo katika kumbukumbu ya mwaka wa pili wa kuuliwa kwake shahidi, ambayo kwa hakika imetokana na nguvu ya Mwenyezi Mungu, imeonesha kwamba, kikokotoo cha Marekani kina dosari na kimeharibika.

Vilevile amegusia mapenzi makubwa ya Waislamu wa madhehebu za Sunni katika nchi tofauti kwa Jamhuri ya Kiislamu na kusema: "Mahafali kubwa za kumuenzi Shahidi Qasem Soleimani katika nchi za Kiislamu ni mfano wa mapenzi na uungaji mkono wa Umma wa Kiislamu kwa Jamhuri ya Kiislamu kuanzia Asia Mashariki hadi Magharibi mwa Afrika.

Aidha amesema mfumo ambao maadui wanatumia kufanya mahesabu yao umevurugika na hawawezi kuwa na tathmini sahihi kuhusu Jamhuri ya Kiislamu na hivyo wataendelea kufeli mara kwa mara.

Ayatullah Khamenei ameendelea kusema kuwa uhasama wa kina wa Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran unatokana na itikadi za kidini.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekutaja "kutosalimu amri mbele ya adui mwenye kiburi na dhalimu" kuwa ni katika misingi ya Mapinduzi ya Kiislamu na kusema: "Kufanya mazungumzo na kuwasiliana na adui katika baadhi ya vipindi hakuna maana ya kusalimu amri mbele yake; kama ambavyo hatujawahi kusalimu amri na wala hatutasalimu amri."

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu  ameashiria watu wanaoitaja kaulimbiu ya "Mauti kwa Marekani" inayotolewa na wananchi wa Iran kuwa ndiyo sababu ya uhasama wa siku zote wa ubeberu dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu na kusema: Marekani ni adui mkubwa wa utawala wa Kiislamu, kwa sababu utawala huo unatokana na dini na ni dhihirisho la itikadi za kidini za wananchi. Amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni dhihirisho na kielelezo cha Uislamu na utawala wa Umma wa Kiislamu.

 

674349

Jina:
Baruapepe:
* maoni:
captcha