IQNA

Umoja wa Mataifa

Rais Raisi: Iran inataka UN ifuatilie jinai ya Marekani ya kumuua kigaidi shahidi Qassem Soleimani

11:31 - September 22, 2022
Habari ID: 3475821
TEHRAN (IQNA)- Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kislamu ya Iran amesema Iran ni mhanga wa ugaidi na amelitaka Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kufuatilia jinai ya kigaidi ya kuuawa shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC).

Shahid Qassem Suleimani  aliuawa katika shambulio la kigaidi la anga la jeshi la Marekani Januari 3, 2020 huko Baghdad Iraq ambalo lilitekelezwa kufuatia amri ya rais wa wakati huo wa Marekani Donald Trump.

Ebrahim Raisi amesema hayo Jumatano katika hotuba yake kwenye mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York na  ambapo pia amesisitiza kuweko uadilifu duniani na kubainisha kuwa, Iran inataka kuweko hatima na mustakabali wa pamoja kwa ajili ya mwanadamu na kwamba, inaunga mkono kuweko dunia yenye uadilifu ndani yake.

Rais wa Iran amesema hamu na shauku ya kutaka kuweko uadilifu ni adia ya Mwenyezi Mungu iko katika dhamira za wanadamu wote.

Rais wa Iran amesisitiza katika hotuba yake hiyo kwamba, Jamhuri ya Kiiislamu ya Iran inaunga mkono kuweko dunia yenye uadilifu, kwani uadilifu unaleta umoja na kwamba, dhulma inachochea na kuleta vita na machafuko.

Rais wa Iran amesema katika sehemu nyingine ya hotuba yake hiyo kwamba, Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yalikuwa ni harakati ya wananchi wa Iran kuelekea ukweli na uhakika, ambapo licha ya kuweko fitina mbalimbali lakini yaliweza kulinda utukufu wa malengo yake.

Kuhusiana na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, Rais Ebrahim Raisi amesema kuwa, Marekani ''ilikanyaga'' na kukiuka makubaliano hayo ya kimataifa yaliyosainiwa mwaka 2015, na kuongeza kuwa Iran haina nia ya kutengeneza  silaha za atomiki kama ambavyo amesisitiza azma ya Tehran ya kuwa na uhusiano mwema na majirani zake wote.

3480586

Jina:
Baruapepe:
* maoni:
captcha