IQNA

Khatibu wa Sala ya Ijumaa Tehran: Iran isimame imara katika mazungumzo ya Vienna

21:46 - January 14, 2022
Habari ID: 3474806
TEHRAN (IQNA)- Khatibu wa Sala ya Ijumaa iliyosaliwa leo hapa mjini Tehran amesema kuwa, adui anaihitajia zaidi Iran katika mazungumzo yanayoendelea mjini Vienna Austria na kusisitiza kuwa, inabidi tusimame imara na kwa ghera katika vita vya kidiplomasia.

Hujjatul Islam Walmuslimin, Mohammad Javad Haj Ali Akbari amesema hayo katika khutba za Sala ya Ijumaa ya leo ya hapa Tehran na kuongeza kuwa, Iran haina haraka katika mazungumzo hayo ya kuondolewa vikwazo ilivyowekewa kidhulma kama ambavyo pia Tehran haitoruhusu mazungumzo hayo yaendelee bila ya kuwa na mwisho.

Khatibu huyo wa muda wa Sala ya Ijumaa ya Tehran vile vile amesema, katika siasa za mambo ya kigeni na wakati taifa lenye ghera la Iran linapoziunga mkono siasa hizo, lazima wanaoshiriki kwenye mazungumzo kama hayo nao wawe imara na wasiogope chochote, wamtegemee Mwenyezi Mungu na waendelee na mchakato wa mazungumzo kwa idili na busara ili kwa njia hiyo waweze kufelisha njama zote za adui.

Awamu ya nane ya mazungumzo ya nyuklia ya namna ya kutekeleza mapatano ya JCPOA na kuondolewa vikwazo vya kidhulma ilivyowekewa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, iliendelea tarehe tatu mwezi huu wa Januari 2022 katika mji mkuu Austria, Vienna. Katika kipindi hiki cha siku 12 za mazungumzo hayo, pande mbili yaani Iran na kundi la 4+1, zimejadiliana masuala tofauti na zote zimesema kuwa mazungumzo hayo yanaendelea vizuri. 

4028455

captcha