IQNA

Sala ya Ijumaa Tehran yaanza tena baada ya kusitishwa kutokana na COVID-19

19:26 - October 22, 2021
Habari ID: 3474457
TEHRAN (IQNA)- Baada ya kusitishwa kwa muda wa takribani miezi ishirini jijini Tehran na katika miji na maeneo mengine ya Iran kutokana na maambukizi ya virusi vya corona, Swala ya Ijumaa imefanyika leo mjini Tehran ikishirikisha matabaka mbalimbali ya wananchi.

Ibada ya Sala ya Ijumaa mjini Tehran ilisimamishwa tangu mapema mwaka jana kutokana na maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19 lakini sasa na kutokana na zoezi la kutoa chanjo linaloendelea kwa kasi hapa nchini na vilevile baada ya mwafaka wa Kamati ya Taifa ya Kupambana na Corona, Sala ya Ijumaa imefanyika leo katika eneo la Chuo Kikuu cha Tehran ikiongozwa na Hujjatul Islam Walmuslimin Muhammad Jawad Haj Ali Akbari.

Katika hotuba zake za Sala ya Ijumaa, Hujjatul Islam Walmuslimin Haj Ali Akbari amesema kuwa, Mtume Muhammad (saw) alitumia stratijia tatu kuu kwa ajili ya kujenga Umma wa Kiislamu na kuongeza kuwa: Stratijia ya kwanza ilikuwa sisitizo lake la udharura wa Umma kuwa na mpaka maalumu mkabala wa ukafiri katika fremu ya kuimarisha nguvu, kuwa na izza na ukakamavu ili kuweza kulinda utambulisho wa Waislamu mbele ya njama za kufru na ukafiri. Amesema stratijia ya pili iliyotumiwa na Mtume SAW kujenga Umma wa Kiislamu ilikuwa kueneza upendo, umoja na mshikamano wa ndani ya Umma. Imamu wa Sala ya Ijumaa ya leo mjini Tehran amesema kuwa stratijia ya tatu ilikuwa kusisitiza kwamba msingi wa jamii ya Kiislamu, umoja na nembo ya mshikamano wake unapaswa kusimama katika kumtaja na kumbumbuka Mwenyezi Mungu na kumwabudu Yeye peke Yake. 

Hatibu wa Sala ya Ijuma ya leo mjini Tehran amesema kuwa, suala la umoja na mshikamano baina ya Waislamu si jambo la kijuujuu tu au mbinu na taktiki, bali ni mkakati na jambo la kimsingi. Ameongeza kuwa jambo muhimu zaidi baina ya Umma wa Kiislamu ni kuunganisha pamoja safu, nyoyo na fikra zao ambavyo vinajumuishwa pamoja katika udugu wa Kiislamu.

Hujjatul Islam Haj Ali Akbari amesema Mwenyezi Mungu SWT amejenga uhusiano huo wa kidugu baina ya Waislamu na amewataka waulinde kwa kupendana na kustahamilia.

Amesisitiza kuwa, matatizo ya ndani ya Umma wa Kiislamu yanapaswa kutatuliwa na Waislamu wenyewe.  

Sala ya Ijumaa Tehran pia imehudhuriwa na wanazuoni kutoka nchi mbali mbali za Kiislamu ambao wako nchini kushiriki Kongamano la 35 la Kimataifa la Umoja wa Kiislamu kwa mnasaba wa Maulid ya Mtume Muhammad SAW na Wiki ya Umoja wa Kiislamu.

4007088

Jina:
Baruapepe:
* maoni:
captcha