IQNA

Kashfa ya kubaguliwa mbunge Muislamu Uingereza

17:26 - January 24, 2022
Habari ID: 3474845
TEHRAN (IQNA)- Kadhia ya chuki dhidi ya Uislamu na kubaguliwa Waislamu katika nchi za Ulaya ikiwemo Uingereza imeshika kasi katika miaka ya hivi karibuni. Chuki hizi dhidi ya Uislamu sasa zimefika hata katika ngazi rasmi za serikali.

Nusrat Ghani naibu wa zamani wa waziri wa uchukuzi Uingereza siku ya Jumapili katika mahojiano na gazeti la Sunday Times alisema aliachishwa kazi hiyo kutokana na kuwa yeye ni Muislamu.

Bi. Ghani ambaye ni mwanachama wa chama tawala cha kihafidhina au Conservative amesema moja wa wananchama wa chama hicho ambaye ni mbunge alimfahamisha kuwa wabunge wenzake hawakupedezwa naye kutokana na kuwa yeye ni mwanamke Muislamu. Ghani amefafanua zaidi kwa kusema: "Mwaka 2020 na kabla ya mabadiliko makubwa katika baraza la mawaziri la Boris Johnson Waziri Mkuu wa Uingereza, nilifahamishwa kuwa kuna wasi wasi kuwa sikuwa mtiifu kwa chama kwa sababu sikukitetea ipasavyo wakati kilituhumiwa kuwa kina chuki dhidi ya Uislamu."

Nusrat Ghani alitimuliwa katika baraza la mawaziri la Uingereza mnamo Februari 2020. Mwaka 2015 Nusrat alichaguliwa kuwa mjumbe katika Bunge la Commons akiwa anawakilisha jimbo la Wealden. Yeye ni Muislamu mwenye asili ya eneo la Jammu na Kashmir linalotawalia na India.

Hivi sasa Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson ametaka uchunguzi ufanyike kuhusu kadhia hii.

Kadhia ya chuki dhidi ya Uislamu ndani ya chama cha Conservative cha Uingereza iliibuka mwaka 2019 wakati ilipobainika kuwa washauri 25 wa chama hicho waliwahi kutuma katika mitandao ya kijamii maudhui za kibaguzi na zilizo dhidi ya Uislamu. Kadhia ilikosolewa vikali sana wakati huo na taasisi za Kiislamu nchini Uingereza ambapo Baraza la Kiislamu la Uingereza (MCB) lilitaka uchunguzi rasmi ufanyika kuhusu chuki dhidi ya Uislamu katika chama tawala wa Conservative.

Kwa mujibu wa Baraza la Kiislamu la Uingereza kumeshuhudiwa kesi nyingi sana za chuki dhidi ya Uislamu katika chama cha Conservative ikiwa ni pamoja na matamshi makali dhidi ya Uislamu yaliyotolewa na Bob Blackman mwanachama wa chama hicho katika Bunge la Commons.

Kwa muda mrefu Blackman amekuwa akieneza chuki dhidi ya Uislamu na hayuko peke yake katika misimamo kama hiyo katika chama cha Conservative. Hivi sasa wanasiasa kadhaa wa chama hicho cha Kihafidhina wanaotaka kushiriki katika uchaguzi wameanza kueneza chuki dhidi ya Uislamu. 

Kinyume na inavyodai serikali ya Kihafidhina ya Uingereza, hivi sasa chuki dhidi ya Uislamu ni sera rasmi ya nchi hiyo katika ngazi za chama na za serikali.

Salman Sayyid Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Leeds anasema: Chuki dhidi ya Uislamu inaongezeka sana Uingereza na sababu kuu ya hilo ni kuwa Waislamu nchini humo wanajitokeza wazi kubainisha utambulisho wao wa Uislamu."

Uchunguzi wa Tume ya Kiislamu ya Haki za Binadamu Uingereza umebaini kuwa asilimia 80 ya Waislamu Uingereza wanakabiliwa na chuki dhidi ya Uislamu.

Aidha takwimu rasmi za Uingereza zinaonyesha kuwa Waislamu ni jamii ya wachache inayokabiliwa na ubaguzi mkubwa zaidi. Takwimu zinaonyesha kuwa kuwa  ni vigumu kwa Waislamu kupata kazi ikilinganishwa na watu wa dini zingine.

Kwa ujumla chuki dhidi ya Uislamu ni jambo ambalo linachukua mwelekeo rasmi Uingereza  na hivi sasa ufichuzi wa Nusrat Ghani kuhusu namna alivyoachiswa kazi kutokana na kuwa yeye ni Muislamu ni jimbo linaloweka wazi ubaguzi  dhidi ya Waislamu katika ngazi za juu katika nchi hiyo.

3477519

captcha