IQNA

Nchi 48 zashiriki Mashindano ya Kimataifa ya Qur’ani Algeria

14:38 - December 30, 2025
Habari ID: 3481739
IQNA – Mashindano ya 21 ya Kimataifa ya Qur’ani nchini Algeria yameanza kwa ushiriki wa wawakilishi kutoka zaidi ya nchi 48.

Tuzo ya Qur’ani ya Algeria imezinduliwa chini ya usimamizi wa Youssef Belmahdi, Waziri wa Masuala ya Kidini na Awqaf wa nchi hiyo, kwa mujibu wa taarifa ya Radio Algeria. Akizungumza na waandishi wa habari, Belmahdi alisema idadi ya nchi zinazoshiriki katika toleo hili, ambalo limefanyika kwa msaada wa Rais Abdelmadjid Tebboune, imefikia 48. Aliongeza kuwa idadi hii inaonyesha ukuaji endelevu wa nafasi ya Tuzo ya Kimataifa ya Qur’ani ya Algeria katika uwanja wa kimataifa.

Kwa mujibu wa Belmahdi, raundi ya awali ya mashindano haya inaandaliwa kwa njia ya mtandao kupitia mikutano ya video katika balozi, konsuli na ofisi za kidiplomasia za Algeria nje ya nchi. Mashindano haya yanafanyika chini ya usimamizi wa jopo la majaji wa kimataifa, wakiwemo majaji wanne kutoka Algeria, mmoja kutoka Syria na mwingine kutoka Oman.

Mashindano haya ni fursa ya kubaini wasomaji wapya na vipaji bora kutoka ndani na nje ya nchi, na pia yanaonyesha maendeleo ya Algeria katika kuhudumia Qur’ani Tukufu kupitia misikiti, shule za Qur’ani na kamati za usomaji, alisema Belmahdi. Aidha, aliongeza kuwa serikali ya Algeria, kwa mujibu wa maelekezo ya rais wa nchi, inaunga mkono mashindano ya kimataifa ya Qur’ani na inatoa kipaumbele maalumu kwa wabebaji wa Kitabu cha Mwenyezi Mungu (wasomaji na wahifadhi) kwa kuanzisha fani mpya na kuongeza thamani ya zawadi za kifedha.

Raundi ya awali ya mashindano haya itaendelea hadi Jumatano, ambapo washiriki 20 kutoka nchi mbalimbali watachaguliwa na kutambulishwa kushindana katika hatua ya mwisho itakayofanyika mwezi ujao.

3495901

Kishikizo: algeria qurani tukufu
captcha