IQNA

Akiwa ameshika Qur’ani Tukufu, Mamdani aandika historia kama meya Mwislamu wa jiji la New York

14:19 - January 01, 2026
Habari ID: 3481747
IQNA – Katika hafla iliyovunja desturi za karne nyingi, Zohran Mamdani alianza rasmi muhula wake kama meya wa Jiji la New York siku ya Alhamisi kwa kuapa akiwa ameshika Qur’an Tukufu, tukio la kihistoria kwa Waislamu na kwa mandhari ya kisiasa ya jiji hilo kubwa.

Mamdani, Meya wa kwanza Mwislamu, mzaliwa wa Uganda mwenye asili ya Asia Kusini katika mji mkubwa zaidi wa Marekani, alitumia Qur’ani  Tukufu ya babu yake pamoja na nakala ya miaka 200 iliyokopwa kutoka Maktaba Kuu ya Umma ya New York (NYPL) katika hafla ya faragha iliyofanyika kwenye kituo cha chini ya ardhi kilichotelekezwa chini ya Times Square.

Ijumaa, anatarajiwa kutumia nakala mbili za Qur’an zilizokuwa mali ya babu na nyanya yake katika sherehe ya mchana itakayofanyika kwenye Jumba la Jiji la New York.

Nakala ya Qur’ani ya kihistoria iliyokopwa kutoka maktaba hapo awali ilikuwa mali ya Arturo Schomburg, mwanahistoria na mwandishi mwenye asili ya Afrika aliyeuza mkusanyiko wake wa vitabu 4,000 kwa NYPL mwaka 1926. Mkusanyiko huo baadaye ukawa kitovu cha Utafiti wa Utamaduni wa Watu Wenye Asili ya Afrika wa Schomburg.

Schomburg alizaliwa Puerto Rico mwishoni mwa karne ya 19 kwa wazazi wa asili ya Kijerumani na Karibi ya Kiafrika. Baadaye alihamia New York na akawa mhimili wa harakati za Harlem Renaissance katika miaka ya 1920 na 1930 – kipindi cha ustawi mkubwa wa kiutamaduni na kiakili miongoni mwa jamii ya Weusi wa New York.

Maktaba ilipongeza uamuzi wa Mamdani kutumia nkala ya Qur’ani ya Schomburg kwa sababu ya uhusiano wake na mmoja wa wasomi mashuhuri wa jiji hilo na kwa unyenyekevu wa ufundi wake. Nakala hiyo ndogo yenye maandiko mekundu na meusi inaashiria ilibuniwa kwa matumizi ya kila siku. Ingawa haijasainiwa wala kutajwa tarehe, maandiko yake madogo ya naskh na jalada lenye medali ya dhahabu iliyopambwa kwa maua vinaonyesha ilitengenezwa Syria ya Kiosmani katika karne ya 19.

Hiba Abid, msimamizi wa masomo ya Kiarabu na Kiislamu, alisema: “Umuhimu wa nakala hii ya Qur’ani  unazidi uzuri wa kurasa zake. Ni nakala ya Qur’an ya karibu na watu, si kwa ufundi wake tu, bali pia kwa kuwa ni sehemu ya hazina ya maktaba kubwa zaidi ya umma nchini.”

Mamdani ni miongoni mwa wanasiasa wachache wa Marekani walioapa kwa Qur’ani Tukufu. Ingawa sheria za New York hazimlazimishi meya kuapa kwa maandiko ya dini, wengi wa waliomtangulia walitumia Biblia. Michael Bloomberg alitumia Biblia ya familia ya miaka 100, Bill de Blasio alitumia Biblia ya Rais wa zamani Franklin D Roosevelt, na Eric Adams alitumia Biblia ya familia yake.

Imani ya Mamdani na asili yake kama Mmarekani aliyezaliwa Uganda mwenye nasaba ya Asia Kusini vilikuwa kiini cha kampeni yake, iliyolenga kusherehekea utofauti wa New York. Katika video zilizovuma mitandaoni, alizungumza kwa uwazi kuhusu athari za mashambulizi ya Septemba 11 na kuongezeka kwa chuki dhidi ya Uislamu nchini Marekani, sambamba na simulizi za maisha ya kila siku ya Waislamu na wahamiaji wa jiji hilo.

Aidha, Mamdani amejitokeza wazi kukosoa sera za Israel dhidi ya Wapalestina na vita vyake vya kikatili huko Gaza.

Wakosoaji wake, akiwemo Mwakilishi Elise Stefanik, walimshambulia kwa misimamo yake ya mrengo wa kushoto kama Democratic Socialist, wakimuita “Mkomunisti wa Jihad” na mfuasi wa “ugaidi.”

Hata hivyo, Mamdani aliahidi kutokuficha asili yake. Katika hotuba ya kampeni alisema: “Sitabadilisha mimi ni nani, wala namna ninavyokula, wala imani ninayojivunia. Sitajificha tena gizani, bali nitajitokeza kwenye nuru.”

3495925

Kishikizo: meya new york mwislamu
captcha