IQNA

Wanawake Waislamu London wanaishi katika hofu ya ubaguzi

21:00 - November 06, 2021
Habari ID: 3474522
TEHRAN (IQNA)- Mwenyekiti wa msikiti mmoja mjini London amebainisha masikitiko yake kuhusu kuongezeka ubaguzi na bughudha dhidi ya wanawake Waislamu.

Mohammad Kozbar, mwenyekiti wa Msikiti wa Finsbury Park katika Barabara ya St Thomas mjini London ametoa wito kwa serikali ya Uingereza kutambua chuki dhidi ya Uislamu au Islamophobia kuwa ni tatizo ambalo liko katika jamii.

Ameongeza kuwa, “Tunapokea taarifa nyingi kutoka kwa wanawake ambao ndio walengwa wakuu wa chuki dhidi ya Uislamu. Wanatambulika kirahisi kuwa ni Waislamu kutokana na kuwa wanavaa Hijabu au mtandio. Wakati mwingine wakihujumiwa huwa hawawezi kujitetea. Wengi wao wanalengwa wakiwa katika maeneo ya umma, wakati wanapelekea watoto shuleni, wakiwa kazini au wakiwa chuo kikuu.”

Aidha anasema hali ni mbaya kiasi kwamba baadhi ya wanawake sasa wanaogopa kutoka nje peke yao kwani wanahisi wanaweza kushamuliwa wakati wowote ule.

Kozbar anasema hali hii imefanywa kuwa mbaya na wanasiasa, akiwemo waziri mkuu Boris Johnson ambaye amewahi kunukuliwa akiwakejeli wanawake Waislamu wanaovaa Hijabu hasa wale wanaovaa niqabu. Anabainisha masikitiko yake kuwa vyama viwili vikuu Uingereza yaani Leba na Conservative, havijachukua hatua yoyote ya kukabiliana na chuki dhidi ya Uislami.

Mwezi Aprili serikali ya Uingereza ilitakiwa itambue rasmi uwepo wa tatizo la chuki dhidi ya Uislamu yaani Islamophobia ili ikabiliane na tatizo hilo.

Kamati ya Bunge kuhusu Waislamu nchini Uingereza imependekeza kutambuliwa rasmi chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu. Katika pendekezo hilo wabunge hao wametaka chuki dhidi ya Uislamu itambuliwe kuwa ‘ni itikadi yenye mizizi ya ubaguzi ambayo inalenga Waislamu au wale wanaodhaniwa ni Waislamu.

Baraza la Uislamu la Uingereza limesema chuki dhidi ya Uislamu imetambuliwa kuwa ni jinai na wabunge na jumuiya za kiraia nchini Uingereza lakini chama tawala cha Wahafidhina au Conservative kimekataa kutambua rasmi uwepo wa tatizo hilo.

Baraza la Uislamu la Uingereza limesema chama cha Conservative kinakana uwepo wa tatizo la chuki  dhidi ya Uislamu miongoni mwa wanachama wake na hivyo hakina hamu ya kutambua uwepo tatizo hilo katika taasisi za Uingereza.

3476366

captcha