IQNA

Kituo Kipya cha Kuhifadhi Qur’ani Chazinduliwa Somalia

15:05 - December 31, 2025
Habari ID: 3481746
IQNA – Kituo kipya cha kuhifadhi Qur’an kimefunguliwa katika eneo la Kahda, jimbo la Banadir, Somalia.

Shirika la Misaada la Qatar (QC) limezindua Kituo cha Amina Cha Kuhifadhi Qur'ani. Hiki ni kituo cha kumi kilichojengwa na QC mwaka 2025 nchini humo kwa msaada wa wafadhili wenye moyo wa kutoa.

Kituo hicho kina vyumba vitatu vya madarasa pamoja na ofisi kamili ya utawala. Jengo limewekewa vifaa vyote muhimu vinavyohitajika kuendesha masomo ya kuhifadhi Qur’ani, kuhakikisha mazingira salama na bora ya kujifunza kwa wanafunzi wa kiume na wa kike.

QC imesisitiza dhamira yake ya kufundisha Qur’ani Tukufu kama sehemu ya miradi yake ya maendeleo katika nyanja za elimu na utamaduni. Hii inajumuisha kujenga, kuandaa na kuendesha vituo vya kufundisha na kuhifadhi Qur’ani. Aidha, QC inalenga zaidi kipengele hiki kupitia mradi wa Furqan unaotekelezwa na mpango wa Rofaqa katika nchi kadhaa, ukilenga hasa mayatima wanaodhaminiwa na mpango huo, hususan katika nchi zisizo za Kiarabu. Mradi huu unalenga kuwafundisha lugha ya Kiarabu na kuboresha ujuzi wao ili waelewe Qur’ani vyema, wajifunze kusoma na kuhifadhi kwa usahihi, na kuimarisha thamani za Kiislamu.

Uzinduzi wa kituo hiki, ambacho ni mchango mkubwa kwa elimu ya Qur’ani nchini Somalia, ulifanyika katika hafla rasmi iliyohudhuriwa na maafisa wa serikali za mitaa, wawakilishi wa Wizara ya Awqaf na Mambo ya Kiislamu, viongozi wa shule, wanazuoni, wazazi na wanafunzi.

Katika hotuba yake, Saadia Ibrahim Abdi, msemaji wa Kituo cha Al-Bashair Cha Kuhifadhi Qur'ani, alitoa shukrani za dhati kwa mfadhili wa Kiqatar aliyefadhili ujenzi wa kituo kwa mchango wake. Pia alisifu juhudi za QC katika kulibadilisha wazo hili kuwa mradi wa kipekee unaohudumia jamii.

Sheikh Abubakr Ali Jabu, mwakilishi wa Wizara ya Awqaf na Mambo ya Kiislamu, alisifu jukumu la QC na mfadhili huyo, akisisitiza kuwa wizara inatoa kipaumbele maalum kwa kuendeleza vituo vya kuhifadhi Qur’an na kuimarisha thamani za Kiislamu.

Kwa upande wake, Abdul Razzaq Muhammad Sheikh Abdullah, afisa wa Kahda, alieleza shukrani zake kwa kufunguliwa kwa kituo hicho, akithibitisha kuwa mradi huu ni “mchango muhimu kwa huduma za elimu katika eneo hili na unasaidia kukuza uwezo wa vijana na kuendeleza elimu ya Kiislamu katika jamii.” Aliongeza kuwa eneo hilo linatarajia miradi zaidi ya maendeleo na elimu itakayoliinua na kukidhi mahitaji ya wakazi wake.

Ufunguzi wa Kituo cha Amina Cha Kuhifadhi Qur'ani umeongeza alama mpya ya kielimu inayohudumia watu wa eneo hilo na kuchangia kuimarisha nafasi ya jamii katika kuhifadhi Qur’ani, kuwapa vijana elimu yenye manufaa, na kuinua kiwango cha elimu na uelewa wa kidini katika jamii.

3495905

Kishikizo: qurani tukufu somalia
captcha