IQNA

Ayatullah Lotfollah Safi Golpaygani kuzikwa katika mji wa Karbala, Iraq

12:17 - February 03, 2022
Habari ID: 3474885
TEHRAN (IQNA)- Mwili mtakatifu wa mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu Ayatullah Safi Golpaygani umehamishiwa katika Msikiti wa Sheikh Tusi karibu na Haram ya Imam Ali bin Abi Twalib (AS) baada ya kuwasili katika mji mtakatifu wa Najaf.

Ayatullah Lotfollah Safi Golpaygani, mmoja wa viongozi wakuu wa kidini katika mji wa Qum nchini Iran, aliaga dunia Jumatatu jioni.

Mwili wa mwanazuoni huyo mkubwa wa Kiislamu pia utazikwa leo, Alhamisi, katika haram ya Imam Hussein AS mjini Karbala baada ya kusindikizwa na waumini katika mji mtakatifu wa Najaf. Ayatullah Safi Golpaygani aliaga Jumatatu akiwa na umri wa miaka 103.

Kwa muda wa miaka mingi, Ayatullah Safi Golpaygani, ambaye alikuwa ni Shaikhul-Maraajii, yaani Marjaa Taqlidi wa hapa nchini mwenye umri mkubwa zaidi, amefundisha katika chuo cha kidini cha Qom na kualifu na kuhakiki vitabu mbalimbali vya Fiqhi, Ilmul-Kalami na Hadithi.

Mwanazuoni huyo aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali za kisiasa ikiwemo ya mjumbe wa Baraza la Wanazuoni Wataalamu Wanaomchagua Kiongozi Mkuu wa Iran na mjumbe wa Baraza la Kulinda Katiba .

Marjaa Taqlidi huyo ameacha athari zaidi 80 za vitabu alivyoalifu, ambavyo baadhi yao vimeshinda tuzo ya Kitabu cha Mwaka cha Wilayat na Kitabu cha Mwaka cha Mahdawiyyat.

Katika ujumbe wake wa salamu za rambirambi, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei umeeleza kuwa: Ayatullah Safi Golpaygani alikuwa mmoja kati ya nguzo za chuo kikuu cha Qum (Hauza) na miongoni mwa vinara wa elimu na amali, na vilevile mmoja kati ya wanazuoni wazoefu zaidi wa kidini.

Amesema katika kipindi cha baada ya Mapinduzi ya Kiislamu, alikuwa mtu aliyetegemewa na kuaminiwa na Imam Khomeini, Mungu awarehemu.

Ayatullah Khamenei aliongeza katika ujumbe wake kuwa: "Ayatullah Safi Golpaygani alikuwa miongoni mwa nguzo kuu za Baraza la Walinzi wa Katiba kwa miaka mingi, na baada ya hapo alishughulikia masuala ya mapinduzi na nchi kwa moyo wa kuwajibika na alinipa ushauri na kunieleza mitazamo na maoni yake mara kwa mara." 

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekitaja kipaji cha ushairi, uwezo mkubwa wa kumbukumbu za kihistoria na kushughulikia masuala ya kijamii kuwa ni miongoni mwa sifa za shakhsia ya mwanazuoni huyo mkongwe na adhimu, ambaye amesema kifo chake ni hasara kubwa kwa jamii ya kielimu na kidini hapa nchini.

Ayatullah Ali Khamenei ametuma salamu za rambirambi kwa familia ya msom huyo na watoto wake, na vilevile kwa marajii na maulama wakubwa wa chuo kikuu cha kidini cha Qum (Hauza), na wafuasi wake hususan katika miji ya Qum na Gopaygani. Vilevile amemuombea rehma na maghufira ya Mwenyezi Mungu. 

4033527

Kishikizo: safi golpaygani marjaa
captcha