Shirika la habari la IRNA limeripoti kuwa, baada ya kuugua kwa muda, Marjaa Taqlidi huyo ameaga dunia kwa ugonjwa wa moyo usiku wa kuamkia leo akiwa na umri wa miaka 103.
Faqihi huyo wa madhehebu ya Ahlubaiti wa Bwana Mtume SAW, alikuwa mmoja wa wanafunzi wakubwa wa Maayatullah Bourujerdi, Hojjat, Khansari na Golpaygani; na aliwahi pia kwenda kuchota hazina ya elimu Najaful-Ashraf nchini Iraq kwa Maayatullah Muhammad Kadhim Shirazi na Muhammad Ali Kadhimi.
Kwa muda wa miaka mingi, Ayatullah Safi, ambaye ni Shaikhul-Maraajii, yaani Marjaa Taqlidi wa hapa nchini mwenye umri mkubwa zaidi, amefundisha katika chuo cha kidini cha Qom na kualifu na kuhakiki vitabu mbalimbali vya Fiqhi, Ilmul-Kalami na Hadithi.
Mwanazuoni huyo aliwahi kushika pia nyadhifa mbalimbali za kisiasa ikiwemo ya mjumbe wa Baraza la Wanazuoni Wataalamu wa Katiba, mjumbe wa Baraza la Kulinda Katiba na akateuliwa na Imam Khomeini (MA) kuwa Katibu wa baraza hilo.
Marjaa Taqlidi huyo ameacha athari zaidi 80 za vitabu alivyoalifu, ambavyo baadhi yao vimeshinda tuzo ya Kitabu cha Mwaka cha Wilayat na Kitabu cha Mwaka cha Mahdawiyyat.
Muntakhabul-Athar, Auqatu-Salah, Bayanul-Usul na Thalaathu Rasail Fiqhiyyah, ni vitabu vingine alivyoandika alimu na mwanazuoni huyo mkubwa.