IQNA

Wabahrain waandamna kulaani safari ya waziri mkuu wa Israel nchini humo

23:45 - February 16, 2022
Habari ID: 3474936
TEHRAN (IQNA)- Waandamanaji wenye hasira nchini Bahrain wameteketeza moto bendera za utawala wa Kizayuni wa Israel kulaani safari ya siku mbili ya waziri mkuu wa utawala haramu wa Israel Naftali Bennet katika nchi hiyo ndogo ya Ghuba ya Uajemi.

Maandamano yamefanyika kote katika nchi hiyo huku waandamanaji wakikanyaga bendera za Israel na kuziteketeza moja na wakiwa wamebeba mabango yaliyoandikwa, ‘Naftali toka nje.’

Maandamano hayo yamejiri huku kukiwa na sheria kali ambazo zimechukuliwa na maafisa wa usalama nchini humo kuzuia  mijumuiko ya kulaani safari ya waziri mkuu huyo.

Naftali Bennet Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni Jumanne alielekea nchini Bahrain kwa mwaliko rasmi wa Hamad bin Isa Aal Khalifa Mfalme wa nchi hiyo. 

Jumuiya ya kitaifa na Kiislamu nchini Bahrain ya Al-Wifaq imeitaja safari ya Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni huko Manama mji mkuu wa Bahrain kuwa ni hiyana ya utawala wa Aal Khalifa kwa watu wa nchi hiyo na kusisitiza kuwa, safari hiyo inakiuka maadili na ni kitendo chenye lengo la kuyachochea mataifa ya Kiarabu na Kiislamu.

Sheikh Hossein al Daei Naibu Katibu Mkuu wa al Wifaq alitoa radiamali yake kwa ziara hiyo ya waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni mjini Manama ambapo amesema, wananchi wa Bahrain wataendelea kutetea na kuunga mkono  malengo ya Palestina na kwamba hawaafiki hatua yoyote ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala ghasibu wa Kizayuni.  

4036731

Kishikizo: bahrain israel naftali
captcha