IQNA

Mtangazaji wa kwanza kuvaa Hijabu katika Televisheni ya Algeria

22:50 - February 18, 2022
Habari ID: 3474944
TEHRAN (IQNA)- Kwa mara ya kwanza katika historia ya Algeria, mwanamke mtangazaji habari amejitokeza akiwa amevaa Hijabu katika televisheni ya kitaifa.

Najwi Jeddi, amesoma habari wiki hii katika televisheni ya kitaifa akiwa amevaa vazi la staha la Kiislamu, Hijabu, na hivyo kumfanya kuwa wa kwanza kufanya hivyo katika historia ya nchi hiyo.

Kwa muda mrefu sera ya Algeria imekuwa ni kutowaruhusu wanawake waliovaa Hijabu kutangaza habari au vipindi katika televisheni mbali mbali nchini humo.

Ingawa hakuna sheria inayowazuia wanawake wanaovaa Hijabu kutangaza katika televisheni, lakini walikuwa hawaruhusiwei kufanya hivyo kutokana na mazoea.

Mwaka 2012, mwandishi habari Nasira Mazhoud alisimamishwa kazi ya utangazaji habari baada ya kusisitiza kuwa lazima avae hijabu akiwa kazini.

Wanawake wengine waliofutwa kazi kwa kusisitiza kuwa wanataka kuvaa Hijabu ni pamoja na  Iman Mahjoubi, Huriya Harath, Susan bin Habib na Naima Majir.

Televisheni ya Qur’ani ya Algeria ndio pekee iliyokuwa ikiwaruhusu wanawake kuvaa Hijabu wakiwa kazini.

Algeria ni nchi ya Kiislamu iliyoko kaskazini mwa Afrika na asilimia 99 ya wakazi wake ni Waislamu.

4037007

captcha