IQNA

Mafunzo ya Qur'ani

Qur'ani Tukufu inasemaje kuhusu kusengenya?

20:10 - July 01, 2022
Habari ID: 3475449
TEHRAN (IQNA)-Baadhi ya madhambi yana athari kubwa sana katika maisha ya kijamii na ya mtu binafsi na katika kumporomosha mtu kiroho na katika kufikia ukamilifu wa kiutu, kama ambavyo baadhi ya amali njema zina taathira kubwa mno pia katika kumjenga na kumuinua mtu kiroho na kimaanawi.

Kusengenya, ni moja ya madhambi ambayo huwa ni utangulizi wa kufanywa madhambi mengine na kuenea maovu katika jamii. Na hilo huthibiti kwa sura hii, kwamba wakati mtu anapotangaza aibu na mabaya ya watu husababisha kuenea maovu na kuyafanya maovu hayo yazoeleke na kutohisika tena kuwa ni kitu kibaya katika jamii.

Je, Qur’ani Tukufu inasema nini kuhusu kusengenya?

Katika aya ya 12 ya Surat Hujurat tunasoma hivi: ‘Enyi mlio amini! Jiepusheni na dhana nyingi, kwani baadhi ya dhana ni dhambi. Wala msipelelezane, wala msisengenyane nyinyi kwa nyinyi. Je! Yupo katika nyinyi anaye penda kuila nyama ya nduguye aliye kufa? Mnalichukia hilo! Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kupokea toba, Mwenye kurehemu.”

Mtume SAW ya kwamba amesema: Katika usiku wa Miraji nilipita katika kaumu moja na kuwaona watu wa eneo hilo wakijikwangua kwa kucha zao. Nikamuuliza Malaika Jibrili: Hawa ni watu gani na kwa nini wanajikwangua namna hii? Jibril akasema:  Hawa ni watu ambao kazi yao ilikuwa ni kusengenya watu wengine na kuharibu heshima za watu kwa kuwasema kwa ubaya. Kwa hakika wengi wetu kutokana na kughafilika au kutoshikamana kikamilifu na mafundisho ya Uislamu, tumetumbukia na kunasa katika dhambi ya kusengenya na kuwaramba visogo watu wengine. Tunapaswa kutambua kwamba, kila ambaye anafanya juhudi za kufichua aibu za watu wengine zilizojificha, Mwenyezi Mungu atamuumbua na kumfedhehesha.

Mafundisho matukufu ya diniya Kiislamu yanatoa miongozo yenye faida kubwa kwa ajili ya kuacha dhambi ya usengenyaji. Miongoni mwa miongozo hiyo ni kwamba: Mtu aliyeamua kutafuta tiba ya ugonjwa wa kusengenya anatakiwa azingatie nukta hii kwamba, badala ya kuhesabu aibu na kasoro za watu wengine, jambo bora kwake yeye ni kufikiria zaidi aibu na kasoro zake mwenyewe. Bwana Mtume Muhammad SAW amesema: "Hongera kwa mtu anayeshughulishwa na aibu zake badala ya aibu za watu".

Katika hadithi iliyopokewa kutoka kwa Bwana Mtume Muhammad SAW imeusiwa kwamba, waumini wanatakiwa wakatae kuchanganyika na kukaa na watu wasengenyaji mpaka watu hao waache tabia yao hiyo. Kwa sababu kujiondoa kwenye kikao au mkusanyiko wowote kwa msingi wa kukataa kujumuika na watu wasengenyaji kunaweza kuwa kinga nzuri sana na yenye taathira kubwa ya kujizuia na dhambi ya usengenyaji, na ni aina mojawapo ya mapambano hasi ya kukabiliana na mambo yanayochochea kufanya dhambi hiyo nzito.

captcha