IQNA

Maoni ya Mufti Mkuu wa Misri kuhusu matumizi ya Akili Mnemba (AI) katika kutoa Fatwa

20:10 - August 09, 2025
Habari ID: 3481058
IQNA – Mufti Mkuu wa Misri amesema kuwa akili mnemba (Artificial Intelligence – AI) haina mamlaka ya kutoa maamuzi ya Kiislamu au fatwa.

Sheikh Nazir Mohammed Ayyad, ambaye pia ni Mkuu wa Sekretarieti ya Makao Makuu ya Fatwa Duniani, amesema katika mahojiano na gazeti la Al-Shorouk la Misri kwamba “Hati ya Cairo kuhusu Akili Mnemba na Utoaji wa Fatwa” imetayarishwa kama rejea ya kwanza ya kimataifa ya kudhibiti matumizi ya teknolojia ya AI katika nyanja ya dini.

Ameeleza kuwa hati hii ni matokeo ya mashauriano ya kina  kati ya wanazuoni wa Kiislamu na watunga sera, pamoja na wataalamu wa teknolojia, sambamba na ushirikiano wa taasisi za dini za kitaifa na mashirika ya kimataifa.

Amesisitiza kuwa fatwa zinazotolewa na AI haziwezi kuchukua nafasi ya fatwa za kibinadamu, kwa sababu fatwa siyo jibu la maandishi pekee au taarifa iliyochukuliwa kutoka hifadhidata.

“Utoaji wa fatwa ni mchakato wa ijtihād ulio changamano unaohitaji akili ya binadamu iliyoelimika na kufundwa, yenye uwezo wa kufahamu maandiko ya Kiislamu kwa kuzingatia uhalisia unaobadilika, na inayoweza kuelewa makusudio ya Sharia pamoja na kupima matokeo yanayoweza kutokea kutokana na hukumu inayotolewa,” amesema Sheikh Ayyad. “Haya si mambo ambayo AI inaweza kuyakamilisha ipasavyo.”

Kwa mujibu wa kiongozi huyo wa Kiislamu, matumizi ya teknolojia ya AI katika nyanja ya utoaji fatwa yana mipaka maalum.

Teknolojia hii inaweza kuwa msaidizi mwenye akili kwa mwanazuoni au mufti, kwa mfano, ikichangia katika ukusanyaji wa taarifa, uchambuzi wa maswali, na upangaji wa fatwa, lakini haina mamlaka ya kutoa maamuzi ya kidini au kutoa fatwa ya mwisho, amesema.

Sheikh Ayyad ameongeza kuwa kuzingatia mipaka hii kutahifadhi thamani ya kibinadamu na maadili ya mchakato wa utoaji fatwa, na kulinda hadhi ya juu ya ijtihād ya kidini dhidi ya madhara yatokanayo na kutegemea teknolojia pekee.

3494164

captcha