Kwa mara ya kwanza katika kipindi cha karibu miongo miwili, mtaalamu wa Qur’an kutoka Iran alialikwa kujiunga na jopo la majaji wa mashindano ya kimataifa ya Qur’an nchini Malaysia. Gholam Reza Shahmiveh, mwalimu na hakimu mkongwe, alihudumu kama jaji katika toleo la 65 la Mashindano ya Kimataifa ya Wasomaji wa Qur’an (MTHQA), yaliyofanyika Kuala Lumpur kuanzia tarehe 2 hadi 9 Agosti.
“Malaysia imekuwa ikiandaa mashindano ya Qur’an tangu mwaka 1960, na kwa historia hii tunaweza kusema wazo la mashindano ya kimataifa ya Qur’an lilizaliwa hapa,” alisema Shahmiveh katika mahojiano na IQNA. “Kabla ya Malaysia, hakukuwa na mashindano kama haya duniani.”
Amesema tukio hili, ambalo sasa linaingia mwaka wa 65, linafanyika kwa kiwango cha juu cha umahiri na mpangilio. “Mashindano haya yamekuwa sehemu ya utambulisho wa kitamaduni wa Malaysia. Waandalizi wamejifunza kuyapanga kwa nidhamu na utaratibu mkubwa,” aliongeza.
Shahmiveh pia alibainisha vipengele viwili muhimu vinavyotofautisha mfumo wa Malaysia. “Kila qari anapaswa kusoma kwa kutumia maqamat manne, kila moja ikiwa na sehemu nne, na usomaji wote usizidi dakika kumi. Hii ni tofauti na mfumo wa Iran, ambapo mipaka ipo zaidi katika maandiko kuliko muda, na msisitizo unakuwa katika utofauti badala ya maqamat maalumu.”
“Lazima tuheshimu mbinu zote na tuwafundishe wasomaji Qur’an ambao wanaweza kukidhi matarajio ya mashindano tofauti duniani kote,” alifafanua.
Kuhusu kiwango cha washiriki, alikiri kwamba ingawa kulikuwa na utofauti wa viwango, wasomaji waliopata nafasi za juu walionyesha kipaji cha kipekee. “Kama ilivyo katika mashindano mengine, baadhi ya washiriki walikuwa dhaifu … lakini ukitazama waliopata nafasi ya kwanza hadi ya sita, ni maqari wenye uwezo mkubwa sana,” alisema.
Mwaka huu, mashindano hayo ya Qur’ani nchini Malayasia yaliwaleta pamoja washiriki 71 kutoka nchi 49, na kuufanya kuwa miongoni mwa mashindano ya kifahari zaidi duniani katika usomaji na hidhi ya Qur’ani.
Katika hafla ya kufunga mashindano tarehe 9 Agosti, Qari Aiman Ridhwan Mohamad Ramlan na Qariah Wan Sofea Aini Wan Mohd Zahidi kutoka Malaysia walitwaa nafasi ya kwanza katika kipengele cha usomaji.
Shahmiveh, mwenye uzoefu wa miongo kadhaa katika kufundisha na kuwa jaji katika mashindano ya Qur’an, alisema kwamba mfumo wa Malaysia unaweza kuwa rejeleo kwa mataifa mengine.
“Hatupaswi kusema njia moja ndiyo sahihi na nyingine siyo. Badala yake, tunapaswa kujifunza kutoka kwao ili tuwaandae wasomaji wetu vizuri kwa jukwaa la kimataifa,” aliongeza.
Katika mashindano haya, Mohsen Qassemi aliwakilisha Iran katika kipengele cha usomaji.
3494265