Awamu hii ya mashindano ya kila baada ya miaka miwili ilifunguliwa rasmi siku ya Jumatatu, ikisimamiwa na jaji mashuhuri wa kimataifa, Abbas Emamjomeh, ambaye pia ni qari mwenye tajriba kutoka Iran.
Washiriki waliagizwa kuchagua sehemu maalum ya Qur'ani na kurekodi video ya dakika tano wakisoma kwa kuzingatia kanuni za mashindano kama zilivyowekwa na waandaaji kutoka Iran.
Kwa mujibu wa waandaaji, jumla ya video 55 ziliwasilishwa, ambapo 45 kati ya hizo zilitimiza masharti ya ushiriki. Video hizi kutoka mataifa 36 sasa zinapitia mchakato wa tathmini ya awamu ya awali kwa njia ya mtandao bila ya kuunganishwa moja kwa moja.
Wale watakaopata alama za juu wataendelea hadi awamu inayofuata ya mashindano.
Mashindano haya yanaratibiwa na Jumuiya ya Qur'ani ya Wasomi wa Iran chini ya Akademia ya Kitaifa ya Iran ya Elimu, Utamaduni na Utafiti (ACECR), na ni mashindano pekee ya kimataifa ya Qur'ani yanayolenga wanafunzi Waislamu pekee. Toleo la kwanza lilizinduliwa mwaka 2006, likiwa ni mwendelezo wa mafanikio ya tamasha 24 za kitaifa za wanafunzi wa Qur'ani nchini Iran.
Mashindano haya pia yanajumuisha kategoria ya kuhifadhi Qur'ani nzima. Awamu ya awali ya sehemu hiyo ilifanyika kwa njia ya mtandao kuanzia Julai 20 hadi Agosti 1, ikiwakilishwa na washiriki kutoka mataifa 47.
Washiriki walisoma mubashara au moja kwa moja kupitia kiunganishi cha video katika Studio ya Mobin ya Shirika la Kimataifa la Habari za Qur'ani (IQNA) mjini Tehran, huku jaji mzoefu Mo’taz Aghaei akisimamia tathmini.
Akizungumza baada ya awamu ya kuhifadhi, Aghaei alisifu kiwango cha juu cha usomaji: “Tulishuhudia mashindano ya kiwango cha juu sana katika awamu ya awali. Baadhi ya washiriki walipata alama kamili, na zaidi ya nusu walipata alama bora kabisa.”
Aliongeza kuwa mkusanyiko wa ubora kama huo ni nadra sana, akisisitiza: “Awamu hii imevuka matarajio.”
Taarifa kuhusu tarehe na mahali pa kufanyika kwa awamu ya mwisho ya mashindano haya zitatangazwa hivi karibuni.
3494301