IQNA

Mikakati ya kusoma Qur'an kwa Njia ya Kidijitali Yazinduliwa Kimataifa Makkah

23:57 - August 05, 2025
Habari ID: 3481040
IQNA – Mfululizo wa miradi ya kipekee ya Qur'an Tukufu imezinduliwa huko Makkah kwa lengo la kuihudumia Kitabu Kitukufu cha Mwenyezi Mungu.

Katibu Mkuu wa Muslim World League (MWL) na Rais wa Jumuiya ya Wanazuoni wa Kiislamu, Sheikh Muhammad Al-Issa, aliongoza uzinduzi huo.

Uzinduzi huo ulihusisha kufunguliwa kwa "Jukwaa la Kwanza la Uratibu kwa Ajili ya Mijukwaa ya Kimataifa ya Usomaji wa Qur'an Kidijitali", pamoja na kutambulishwa kwa "Lango Kuu la Kidijitali la Usomaji wa Qur'an Kimataifa", na kuanzishwa kwa chama cha kwanza duniani kilichojitolea kwa ajili ya usomaji wa Qur'an kwa njia ya kidijitali.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na wanazuoni mashuhuri, watafiti, na wataalamu wa tajwīd (usomaji sahihi wa Qur’an) na elimu ya Qur’an, pamoja na wawakilishi kutoka zaidi ya majukwaa 50 ya usomaji wa Qur’an kwa njia ya mtandao duniani kote.

Tukio hili lilisisitiza juhudi za hali ya juu za kufundisha na kusoma Qur’an kwa umbali kupitia teknolojia za kisasa za mawasiliano, kwa lengo la kuwafikishia Waislamu elimu ya Qur’an popote walipo.

Sheikh Al-Issa aliwakaribisha wageni, akieleza kuwa mikakati hii inaendana na dhamira ya MWL ya kuimarisha umoja wa Ummah wa Kiislamu na kuutumikia Qur'an Tukufu.

Kwa niaba ya majukwaa shiriki, Dkt. Ahmad Jamil kutoka Indonesia alisifu dira ya kielimu na kiteknolojia ya MWL katika kuunganisha ulimwengu na Qur'an, na kuwezesha kujifunza na kuimudu kwa mujibu wa misingi iliyowekwa na Mashari’a.

Vipindi vinne vya jukwaa hilo vilijadili mada muhimu kama vile:

  • kanuni na taratibu za kutoa ijazah (cheti cha usomaji wa Qur’an) kwa njia ya kidijitali,

  • uundaji wa zana za kufundishia Qur’an kwa umbali,

  • uratibu wa juhudi za kimataifa katika usomaji wa Qur’an kwa njia ya mtandao,

  • na uwasilishaji wa miradi ya ubunifu inayotumia teknolojia katika ufundishaji wa Qur’an.

Miongoni mwa mapendekezo muhimu ya jukwaa hilo ni kuanzishwa kwa "Jumuiya ya Kimataifa ya Majukwaa ya Usomaji wa Qur'an Kidijitali" chini ya usimamizi wa MWL, kama chombo cha kimataifa kitakachoratibu na kukuza usomaji wa Qur’an kwa njia ya kidijitali.

3494113

 

captcha