Kwa mujibu wa Times of India, Fathima ametumia takriban saa 2,416 kukamilisha nakala ya mkono ya juzuu zote 30 za Qur’ani kwa kaligrafia.
Msanii huyo, aliyesomea katika Chuo cha Wanawake cha Markazul Huda (Kumbra), alianza mradi huu Januari 2021 wakati wa zuio la Covid-19, akihimizwa na wazazi wake.
Kazi hiyo ilihitaji kukaa katika mtindo mmoja kwa muda mrefu na kuhakikisha mwandiko unalingana kwenye kurasa zote.
Kwa mujibu wa baba yake, doa la wino liliharibu baadhi ya kurasa za mwanzo na kumlazimu kuanza upya.
Aliendelea tena Oktoba 2024 na kukamilisha kazi hiyo Agosti 2, 2025.
Mchakato mzima ulijumuisha siku 302 za kuandika, ambapo kila ukurasa ulichukua wastani wa saa nne.
Msahafu huo una jumla ya kurasa 604 zilizoandikwa kwa mkono kwenye karatasi nyeupe, buluu nyepesi na kijani kibichi nyepesi, maandiko yakiwa kwa Kiarabu kwa wino mweusi. Msahafu huo una mapambo mekundu na ya dhahabu, na una uzito wa kilo 13.8 ukiwa na vipimo vya inchi 22 kwa 14 kwa 5.5.
Sherehe rasmi ya kuzindua Msahafu huo ilifanyika katika chuo chake Jumamosi.
Uzinduzi ulifanywa rasmi na Murris Yaseen Sakhafi Al Azhari kutoka Markaz Knowledge City, Kerala, mbele ya wanazuoni na wawakilishi wa chuo hicho.
Familia yake imesema wamepokea maombi ya kuonesha nakala hiyo hadharani na wataamua namna ya kuihifadhi baada ya kushauriana na wazee na wanazuoni. Pia wanazingatia kuiwasilisha kwenye Limca Book of Records.
3494312