IQNA

Wamalaysia watumia njia ya heshima ya kuweka mbali Misahafu iliyochakaa

16:48 - August 16, 2025
Habari ID: 3481094
IQNA – Jimbo la Sarawak, Malaysia limeanzisha mbinu rafiki kwa mazingira katika kuheshimu na kuondosha nakala zilizochakaa za Misahafu au Qur’an Tukufu.

Mbinu hii inatumia mifuko maalumu yenye kuzingatia utunzaji mazingiro ambayo huyeyuka baharini; njia ambayo hudumisha heshima ya kidini sambamba na kuhifadhi mazingira.

Hafla ya kuondosha misahafu hiyo ilifanyika Jumatano katika gati ya Bintulu Port Jetty, ikiongozwa rasmi na Mufti wa Sarawak, Datu Kipli Yassin.

Tukio hili liliandaliwa kwa ushirikiano wa Bodi ya Ustawi wa Kiislamu ya Bintulu, Idara ya Dini ya Kiislamu Sarawak (JAIS) pamoja na taasisi kadhaa husika.

Kwa mujibu wa taarifa ya Kitengo cha Mawasiliano ya Umma Sarawak (Ukas), Mufti Kipli alisema kuwa ubunifu huu haudhuru mfumo wa viumbe vya baharini.

“Mifuko hii ya karatasi huyeyuka kabisa ndani ya maji ya bahari. Ubunifu huu ni dhamana kwamba bahari zetu zitabaki salama kwa vizazi vijavyo. Kuheshimu Qur’an si tu kulinda utukufu wake, bali pia ni kudhihirisha kanuni za uendelevu wa mazingira,” alisema.

Aidha, Kipli alisema kuwa Sarawak imepata kutambuliwa kwa hatua hii, akieleza kuwa ni hatua ya kimaendeleo inayounganisha teknolojia na mila na desturi za Kiislamu.

Alithibitisha pia kuwa mbinu hiyo inazingatia mwongozo wa Baraza la Kitaifa la Fatwa, na hivyo kuhakikisha mchakato wote wa kuondosha misahafu unafanyika kwa heshima na umakini mkubwa.

Alipendekeza kuwa njia hii inaweza kuanzishwa kama utaratibu rasmi wa utekelezaji (SOP) katika Sarawak yote, lakini akasisitiza umuhimu wa mshikamano wa wadau wote kuhakikisha utekelezaji wake unafanyika kwa nidhamu na usahihi.

 

/3494257

Habari zinazohusiana
Kishikizo: malaysia qurani tukufu
captcha