Mamlaka ya eneo hilo takatifu ilitangaza Jumapili kuwa idadi ya jumla ya wafanyaziyara walioadhimisha Arbaeen ya mwaka 1447 Hijria ilifikia 21,103,524. Mwaka uliopita idadi ilikuwa 21,480,525.
Maafisa walisema hesabu hiyo ilifanywa kupitia mfumo wa kielektroniki unaotumia Akili Mnemba (AI) uliowekwa barabarani kuelekea Karbala na kwenye malango ya haram ya Abbas ibn Ali (AS).
Kamati Kuu ya Iraq ya Mijumuiko ya Kidini iliripoti kuwa nchi hiyo iliwakaribisha zaidi ya wafanyaziyara wa kigeni milioni 4, pamoja na mamilioni ya wananchi wa Iraq.
Kamati hiyo ilibainisha kuwa usimamizi wa barabara, uliosaidiwa na mifumo ya rada kwenye barabara kuu za kimataifa, ulipunguza ajali za barabarani kwa asilimia 26, vifo kwa asilimia 55, na majeruhi kwa asilimia 36 ikilinganishwa na mwaka uliopita.
Aidha, kamati ilisema Karbala ilitangazwa kuwa “mji usio na silaha” wakati wa ziara hiyo, hatua iliyoongeza hali ya usalama. Iliripoti kupungua kwa visa vya moto kwa asilimia 87, ambapo ni visa vitano pekee vilivyorekodiwa, na ikasifu uratibu wa hali ya juu kati ya vyombo vya usalama na intelijensia.
Waziri wa Ndani wa Iraq, Abdul Amir al-Shammari, ambaye alikuwepo Karbala wakati wa ziara ya Arbaeen, alisema kuwa mpango wa usalama “ulifanikishwa ipasavyo.” Aliongeza kuwa vikosi vya usalama vilipelekwa kwenye njia zote zinazoelekea Karbala, na kulikuwa na ulinzi mkali zaidi kuzunguka haram za Imam Hussein (AS) na Hazrat Abbas (AS) pamoja na maeneo ya mikusanyiko ya wafanyaziyara.
Ziara ya Arbaeen, mojawapo ya mikusanyiko mikubwa zaidi ya kidini duniani kila mwaka, huadhimisha siku ya arubaini baada ya Ashura, kumbukumbu ya shahada ya Imam Hussein (AS), mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW), katika mwaka wa 61 Hijria Qamaria.
/3494261