Katika taarifa rasmi iliyotolewa kufuatia ripoti kwamba baadhi ya taasisi za kisiasa na huduma zimeweka mabango yenye picha ya Ayatullah Sistani katika miji mbalimbali, asa kando ya njia inayotumiwa na wafanyaziyara wanaoelekea katika maqam au Haram takatifu ya Imam Hussein (AS), ofisi yake imeeleza kutoridhishwa na kitendo hicho.
“Tumeona kuwa baadhi ya taasisi za kisiasa na huduma zinatumia picha ya Ayatullah Sistani katika mabango yaliyo wekwa wazi, hasa katika msimu wa hija ya Arbaeen,” taarifa hiyo ilisema.
“Tunasisitiza tena msimamo wetu wa kupinga jambo hili, na tunatoa wito kwa wote kujiepusha na hatua kama hizi. Pia tunazitaka taasisi husika zichukue hatua mwafaka kuhusu suala hili.”
Ayatullah Sistani anahesabiwa kuwa kiongozi wa juu kabisa wa madhehebu ya Shia nchini Iraq, na mchango wake katika kulinda uthabiti wa taifa hilo umetambuliwa kimataifa.
Kadri siku ya Arbaeen inavyokaribia, maelfu ya Waislamu wa madhehebu ya Shia kutoka nchi mbalimbali wanaelekea Iraq kushiriki katika msafara wa pamoja na Wairaqi kutoka kila pembe ya nchi hiyo.
Arbaeen ni tukio la kidini linaloadhimishwa na Waislamu wa Shia katika siku ya arobaini baada ya Ashura, siku ya kumbukumbu ya kuuawa shahidi kwa Imam Hussein (AS), mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW) na Imamu wa tatu wa Waislamu wa madhehebu ya Shia.
Ni moja ya mikusanyiko mikubwa zaidi ya mahujaji duniani, ambapo mamilioni ya Waislamu wa Shia, pamoja na baadhi ya Waislamu wa Sunni na hata wafuasi wa dini nyingine, hutembea kwa miguu kuelekea Karbala wakitokea miji mbalimbali ya Iraq na nchi jirani. Mwaka huu, siku ya Arbaeen itasadifiana na tarehe 14 Agosti.
3494109