Waislamu milioni moja leo wamekusanyika katika mji mtakatifu Makka nchini Saudi Arabia kwa ajili ya Hija. Idadi hii bado ni ndogo ikikumbukwa kuwa kabla ya janga la corona Waislamu milioni 2.5 waliweza kutekeleza ibada ya Hija mwaka 2019.
Kwa mujibu wa kanuni zilizowekwa na Saudia, wale wanaotekeleza ibada hiyo mwaka huu lazima wawe na umri wa chini ya miaka 65, wapate chanjo dhidi ya virusi vya corona na wawe wamepimwa hawana COVID-19 ndani ya saa 72 kabla ya usafiri.
Maafisa wa Saudia walikagua eneo hilo takatifu siku ya Jumatano na kusisitiza "utayari" wao wa kupokea Mahujaji huku wakisisitiza kuhusu ulazima wa "kudumisha afya ya umma."
Baada ya kunza janga la corona mwaka 2020, viongozi wa Saudia waliruhusu Mahujaji 1,000 tu ambao tayari wanaishi katika ufalme huo kuhudhuria.
Mwaka jana, Hija vile vile iliwekewa vikwazo ambapo ni Waislamu 60,000 waliokuwa na chanjo kamili wanaoishi Saudi Arabia ndio walopata idhini ya kutekeleza ibada ya Hija. Vizuizi hivyo ambavyo havijawahi kushuhudiwa vilileta mshtuko katika ulimwengu wote wa Kiislamu, na kuwaumiza waumini wengi ambao walikuwa wametumia miaka mingi kuweka akiba kwa ajili ya ibada ya kidini.
Mwaka huu, hata hivyo, viongozi wa Saudi wamelegeza vizuizi vilivykuwepo kutokana na corona.
Kabla ya corona Hija na Hija Ndogo au Umraha zilileta dola bilioni 12 na hivyo kufanya safari hizo za kidini kuchangia asilimia kubwa ya pato la ndani la Saudi Arabia baada ya mafuta ya petrol.
Ingawa katika siku za hivi karibuni maambukizi ya corona yameongezeka kwa kasi hadi zaidi ya 500 kwa siku nchini Saudi Arabia, serikali imeondoa agiza la kulazimisha uvaaji barakoa na tahadhari zingine za virusi mwezi uliopita. Takriban asilimia 70 ya wakazi wa Saudia wamechanjwa dhidi ya virusi vya corona.
Pamoja na kuwa sheria kali za kuzuia maambukizi ya corona zimeondolewam, hata hivyo, Waislamu bado wamekatazwa kubusu au kugusa Kaaba Tukufu wakati wanapotufu au kuzunguka eneo hilo takatifu.
Qur’ani Tukufu inasema kwamba Waislamu wote ambao wana uwezo wa kimwili na kifedha wanapaswa kuhiji mara moja katika maisha yao. Mahujaji husafiri kwenda Makka kutoka kote ulimwenguni kwa siku tano za ibada.
Waislamu hutekeleza Hija kama alivyotekeleza Mtume Muhammad (SAW) karibu miaka 1,400 iliyopita na inaaminika Hija ya sasa inafuata nyayo za Manabii Ibrahim na Ismail (amani juu yao).
3479608