IQNA

Vita dhidi ya ugaidi

Umoja wa Mataifa watakiwa kutumia jina 'Daesh' kwa kundi husika la kigaidi

16:53 - August 10, 2022
Habari ID: 3475603
TEHRAN (IQNA) - Mashirika ya Umoja wa Mataifa yametakiwa kuacha kutumia neno 'Dola la Kiislamu' yanapotaja kundi la kigaidi la Daesh au ISIS.

Akizungumza katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mjini New York, Balozi wa UAE na Naibu Mwakilishi Mkuu, Mohamed Abushahab, alisisitiza kuwa magaidi hao hawapaswi kuhusishwa na dini ya Kiislamu.

Alisema katika hotuba yake kwamba mashirika hayapaswi "kuruhusu Daesh na vikundi vingine kuteka nyara dini ya kuvumiliana,"  na kuongeza kuwa kuliita kundi la kigaidi la Daesh kuwa eti ni 'Dola la Kiislamu' kutazidi kulipa itibari kundi hilo ovu.

"Ugaidi hauna uhusiano wowote na Uislamu," aliongeza.

Kauli ya Abushahab imekuja huku Umoja wa Mataifa ukitambua kuwa tishio la Daesh na washirika wake limesalia kuwa la kimataifa na linabadilika.

"Daesh na washirika wake wanaendelea kutumia mienendo ya migogoro, udhaifu wa utawala na ukosefu wa usawa ili kuchochea, kupanga na kuandaa mashambulizi ya kigaidi," mkuu wa Umoja wa Mataifa wa kukabiliana na ugaidi Vladimir Voronkov, alisema alipokuwa akiwasilisha ripoti ya kumi na tano ya Katibu Mkuu.

Abushahab alisisitiza kuwa mapambano dhidi ya ugaidi hayahusiana na  Daesh tu, kwani ‘mapambano dhidi ya Al-Qaeda yanasalia kuwa kipaumbele cha kimataifa’ hasa baada ya ‘shirika hilo kuingia katika ombwe la uongozi, kufuatia kifo cha Ayman Al-Zawahiri.’

Wakati wa hotuba yake, alisema teknolojia inaweza kuwa "upanga wenye ncha" na unaweza kutumika kuboresha hali ya maisha ya watu kwa namna moja, lakini kutumiwa vibaya na makundi ya kigaidi katika upande mwingine.

Abushahab alisema 'teknolojia zinazoibuka zina uwezo mkubwa wa kusaidia katika juhudi za kuzuia kukabiliana na ugaidi.'

Alihitimisha matamshi yake kwa kuitaka jumuiya ya kimataifa ‘kuchangamkia fursa hii na kuchukua hatua sasa’ ili kukomesha Daesh na makundi mengine ya kigaidi.

3480043

Kishikizo: ugaidi ، daesh au isis ، uislamu
Jina:
Baruapepe:
* maoni:
captcha