Raisi ameyasema hayo alipokuwa akihutubia kwenye gwaride la kuadhimisha Siku ya Jeshi la Kitaifa mjini Tehran siku ya Jumanne, ambapo amesisitiza kuwa uwezo wa Jeshi la Iran unatokana na ujuzi wa ndani ya nchi.
Rais Raisi ameongeza kuwa: "Maadui, haswa utawala wa Kizayuni (Israel), wamepokea ujumbe kwamba hatua yoyote ndogo ya uchokozi dhidi ya nchi ya Iran itakabiliwa na jibu kali kutoka kwa jeshi na itaambatana na uharibifu wa Haifa na Tel Aviv."
Aidha amesema ujumbe wa Jeshi la Iran kwa wanajeshi wa Marekani ni kwamba lazima waondoke katika eneo la Asia Magharibi haraka iwezekanavyo.
Rais wa Iran amesisitiza kuwa, "vikosi vya majeshi ya nje ya kanda vikiwemo vya Marekani vinapaswa kuondoka katika eneo hili haraka iwezekanavyo kwa sababu ni kwa maslahi yao na kwa maslahi ya kanda." Ameongeza kuwa: "Kuwepo kwa vikosi ajinabi katika kanda ya Asia Magharibi kunatishia usalama wa kikanda lakini vikosi vyetu vya kijeshi vinaimarisha usalama popote vinapokuwa katika kanda hii."
Amebainisha kuwa, Jeshi la Iran limekabiliana na magaidi na kuimarisha usalama katika eneo, huku vikosi vya kigeni vikiwa vinatishia mataifa ya kanda hiyo.
Rais wa Iran amesema nguvu ya Jeshi la Iran ina manufaa kwa usalama wa eneo la Magharibi mwa Asia na "sio siri kwa mtu yeyote kwamba vikosi vyetu vya jeshi vimelinda mipaka na usalama wa nchi za eneo hili,"
Amesisitiza kuwa uwepo wa wanajeshi wa nchi za kigeni, haswa Waamerika, kamwe hakutalinda usalama wa eneo la Ghuba ya Uajemi.
4134959