IQNA

Uchambuzi

Sababu za kurejea Syria katika Jumuiya ya Nchi za Kiarabu

20:15 - May 09, 2023
Habari ID: 3476982
TERHAN (IQNA)- Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za Kiarabu walikubaliana katika mkutano wao waliofanya Jumapili tarehe 7 Mei mjini Cairo kurejeshwa Syria katika Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League), baada ya kusimamishwa uwanachama wake kwa muda wa takriban miaka 12.
Katika rasimu ya uamuzi huo, ambayo itachapishwa rasmi hapo baadaye imeelezwa kuwa: "kuanzia leo Mei 7, ushiriki wa wajumbe wa Syria katika mikutano ya jumuiya hii utaanza tena".
Uamuzi huo wa sasa uliotangazwa na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu unatafautiana kikamilifu na msimamo wa huko nyuma uliochukuliwa na jumuiya hiyo kuhusiana na Syria.
Miezi michache baada ya kuanza mgogoro wa Syria, tarehe 12 Novemba 2011, baadhi ya nchi za Kiarabu ikiwemo Qatar na Saudi Arabia zilitoa mwito wa kusimamishwa uwanachama wa Syria katika mikutano ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu. Kisingizio kilichotolewa na nchi hizo kuondoa kiti cha Syria katika mikutano ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kilikuwa ni tuhuma kwamba serikali ya Damascus inawakandamiza raia wake. Baadhi ya nchi za Kiarabu zilisimamisha na kufunga ofisi zao za uwakilishi wa kisiasa na hata balozi zao ndogo nchini Syria.
Miaka 12 ya mgogoro Syria

Hivi sasa, baada ya kupita karibu miaka 12 tangu ulipoanza mgogoro huo na kushindwa kwa kampeni kubwa ya kuipindua na kuisambaratisha serikali halali ya Syria na rais wa nchi hiyo Bashar al-Assad kuweza kuendelea kubaki madarakani, Jumuiya ya Waarabu, katika mkutano wake wa ngazi ya mawaziri, imechukua uamuzi rasmi wa kuondoa usitishaji wa uwanachama wa Damascus na kuridhia kurejea Syria kwenye jumuiya hiyo. Juhudi hizi zilianzishwa tangu miaka miwili nyuma, ambapo kwa muda wote huo suala la kurejea Syria katika Jumuiya ya Nchi za Kiarabu limekuwa likizungumziwa na kukaririwa mara kwa mara.

Nukta muhimu ni kwamba, jumuiya yenyewe ya Waarabu ndiyo iliyotaka Syria irejeshwe kwenye taasisi hiyo. Baadhi ya viongozi wa Syria wamesema, wao hawakuomba nchi yao irejeshewe uwanachama wake, bali ni nchi za Kiarabu zenyewe ndizo zilizoibua takwa hilo. Sasa kama Damascus sio iliyong'ang'ania au kuomba irejeshwe katika Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, suali ni je, ni Syria ndiyo inayorudi kwenye Jumuiya ya Waarabu sasa hivi au Jumuiya ya Waarabu ndiyo inayorudi kwa Syria?
 
Utabiri uliotimia wa Rais Bashar al-Assad

Kinachotoa mguso zaidi ni kwamba, katika miaka ya mwanzo ya mgogoro wa Syria, wakati nchi kadhaa za Kiarabu zilipovunja uhusiano wao wa kisiasa na Damascus, Bashar al-Assad alisisitiza katika moja ya hotuba zake kwamba, muda si mrefu nchi za Kiarabu zitarejea Syria. Inavyoonekana, siku ambayo Rais Assad aliizungumzia imewadia; na hivi sasa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu inarejea Syria.

Wakati huo huo, kurejea Syria katika Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kunachukuliwa kuwa hatua inayoendana na harakati ya pamoja ya nchi za Kiarabu ya kurejesha uhusiano wa kawaida na Damascus baada ya kufeli kwa kampeni ya pamoja ya muungano wa nchi za Magharibi na za Kiarabu ulioongozwa na Marekani ya kuipindua serikali ya Syria na kumuondoa madarakani Rais Bashar al-Assad. Ulipoanza mgogoro wa Syria mwaka 2011, Saudi Arabia na baadhi ya nchi za Kiarabu waitifaki wa Magharibi zilikuwa kwenye kambi ya waungaji mkono wakuu wa makundi ya kigaidi yaliyoipinga serikali ya Syria na zikaamua kuvunja uhusiano wao na nchi hiyo kwa kufunga balozi zao huko Damascus. Hata hivyo, baada ya kushindwa waziwazi makundi ya kigaidi nchini Syria, na baada ya kupita zaidi ya muongo mmoja, nchi hizo zimefikia hitimisho kwamba kuendelea kufuata njia hiyo na mdundo wa ngoma inayopigwa na nchi za Magharibi sambamba na kupunguza uhusiano wao na Syria hakuna manufaa yoyote kwao wao, bali zinapaswa kuanzisha uhusiano mpya na Serikali ya Syria.
 
Marekani inapinga umoja wa nchi za Kiarabu
Pamoja na hayo, juhudi hizo za pamoja zilizofanywa na nchi za Kiarabu kwa lengo la kurejesha uhusiano na Damascus zimepingwa vikali na Marekani. Serikali ya Joe Biden, kama zilivyokuwa serikali za kabla yake nchini Marekani, inataka serikali halali ya Syria isambaratike na kwa hivyo inapinga hatua zozote zitakazopelekea kutambuliwa au kupata nguvu zaidi serikali hiyo. Lakini licha ya msimamo huo wa Washington, nchi za Kiarabu waitifaki wa Marekani, ambazo hapo awali zilikuwa na msimamo wa pamoja wa kutaka kuipindua serikali halali ya Syria, zimebadilisha waziwazi muelekeo wao wa awali  na kuchukua hatua ya kufufua uhusiano wao wa kidiplomasia na kiuchumi na serikali ya Bashar al-Assad. Nchi kama Muungano wa Falme za Kiarabu-Imarati na Saudi Arabia, ambazo hapo kabla zilikuwa bega kwa bega na Marekani katika njama ya kutaka kumuondoa madarakani Bashar al-Assad, sasa zimebaini kuwa sera na hatua za kambi ya Wamagharibi na Waarabu kwa ushirikiano na Uturuki katika suala hilo zimeshindwa na kugonga mwamba kikamilifu; na makundi ya kigaidi ziliyokuwa zikiyaunga mkono na kushirikiana na Marekani katika kuyazatiti kwa fedha, vifaa na silaha ili kuipindua serikali halali ya Syria, yameshaangamizwa na yaliyobaki hivi sasa, tena huku yakijikongoja kwa uungaji mkono yanaopata kwa Uturuki na Magharibi ni mabaki yao yaliyosalia kwenye mkoa wa Idlib nchini Syria. 
 
Uhalisia mpya wa mambo
 
Nchi nyingi zilizovunja uhusiano na Syria sasa zinakaribisha kurejea Bashar al-Assad baada ya kubainikiwa na uhalisia mpya wa mambo, na hii ni licha ya upinzani unaoendelea kuonyeshwa na Marekani dhidi ya serikali yake..
Kuhusiana na hilo, Imarati, Bahrain na Oman zimeshafungua tena balozi zao huko Damascus, na Saudi Arabia, Jordan, na Misri zinaendelea kufanya mashauriano na Syria kwa ajili ya kurejesha uhusiano wa kawaida, na tayari kuna hatua kubwa zimepigwa katika suala hilo. Mchakato wa kurejeshwa uhusiano wa kawaida kati ya Syria na Iraq na Lebanon nao pia unaendelea, huku Tunisia nayo ikithibitisha kuanzishwa uhusiano wa kisiasa baina yake na Syria.
4139520
captcha