IQNA

Siasa

Yemen: Jumuiya ya Nchi za Kiarabu iko chini ya ushawishi wa Marekani

20:48 - May 21, 2023
Habari ID: 3477025
TEHRAN (IQNA)- Wizara ya Mambo ya Nje ya Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen imekosoa taarifa ya kikao cha Jumuiya ya Nchi za Kiarabu iliyotolewa jana Jumamosi na kusisitiza kuwa, hakuna matumaini ya kuifanyia mageuzi na marekebisho jumuiya hiyo.
Kwa uungaji mkono wa Marekani, Muungano wa Falme za Kiarabu na nchi nyingine kadhaa, mnamo Machi 2015 Saudi Arabia ilianzisha uvamizi na mashambulio ya kijeshi dhidi ya Yemen na kuiwekea mzingiro nchi hiyo wa nchi kavu, baharini na angani.
Moto wa vita uliowashwa na Saudia na waitifaki wake ndani ya Yemen, hadi sasa umeshaua zaidi ya watu 16,000, kuwajeruhi maelfu na kuwafanya wakimbizi mamilioni ya raia wengine wa nchi hiyo.
Kwa miaka kadhaa, Jumuiya ya Nchi za Kiarabu imekuwa ikiunga mkono vita vilivyoanzishwa na Saudia dhidi ya Yemen na kunyamazia kimya uchokozi wa muungano wa kijeshi unaoongozwa na Riyadh.
Kwa mujibu wa chaneli ya habari ya al-Masira, Wizara ya Mambo ya Nje ya Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen imeeleza katika taarifa kwamba kikao cha sasa cha Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kuhusiana na vita vilivyoanzishwa na nchi vamizi za muungano wa Saudia na Imarati dhidi ya Yemen hakina tofauti yoyote na vikao vingine vya jumuiya hiyo; na taarifa iliyotolewa kwenye kikao hicho kwa anuani ya "Taarifa ya Jeddah" nayo pia imevitaja vita dhidi ya Yemen kuwa ni mgogoro na si uvamizi.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Yemen imesisitiza kuwa, muungano wa Saudia umefanya uvamizi na kuweka mzingiro wa kidhalimu dhidi ya taifa la Yemen uliogeuka kuwa hali mbaya zaidi ya kibinadamu katika historia ya zama hizi.
Taarifa ya wizara hiyo imebainisha kuwa, taarifa ya Jeddah imesisitiza juu ya ulazima wa kukomeshwa uingiliaji wa kigeni katika masuala ya ndani ya nchi za Kiarabu, ilhali nchi za muungano wa Saudia zinaingilia waziwazi masuala ya ndani ya Yemen kwa mwaka wa tisa mfululizo.
Sana'a imesisitiza mwishoni mwa taarifa ya wizara yake ya mambo ya nje kwamba kuifanyia marekebisho na mageuzi Arab League na kustawisha shughuli za pamoja za Waarabu ingali ni ndoto isiyoweza kufikiwa kwa sababu Marekani ina satua na ushawishi mkubwa ndani ya jumuiya hiyo.

/4142134

captcha