IQNA

Sura za Qur’ani Tukufu /95

Uumbaji wa wanadamu katika umbo lilio bora kabisa

13:55 - July 15, 2023
Habari ID: 3477285
TEHRAN (IQNA) – Katika baadhi ya aya za Qur’an kama vile Aya ya 4 ya Surah At-Tin, Mwenyezi Mungu anasema amemuumba mwanadamu katika umbo bora kabisa, na hivyo ni juu ya kila mtu mwenyewe kutenda mambo mema zaidi ili kufikia uwezo uliomo ndani yake.

At-Tin ni sura ya 95 ya Qur’ani Tukufu ambayo ina aya 8 na iko katika Juzuu ya 30. Ni Makki na ni Sura ya 28 iliyoteremshwa kwa Mtukufu Mtume (SAW).

Jina la Sura linatokana na neno at-Tin (mtini) na Mwenyezi Mungu anaapa kwa mti huu katika Aya ya kwanza.

Ni miongoni mwa sura za Qur’ani Tukufu zinazoanza kwa kuapa. Katika aya za mwanzo za Surah At-Tin, Mungu anaapa kwa vitu vinne: mtini, mizeituni, ardhi ya Tur (Sinai) na mji mtakatifu wa Makka. Mtini umetajwa katika Qur’ani  Tukufu mara moja wakati mzeituni umetajwa mara sita.

Mada kuu ya Surah At-Tin ni suala la Ufufuo katika siku ya Kiyama, tathmini ya vitendo vyamwanadamu na malipo kwa waja wema  kutoka kwa Mwenyezi Mungu  kesho Akhera.

Sura inaangazia uumbaji wa mwanadamu katika umbo bora zaidi “Bila ya shaka tumemuumba mtu kwa umbo lilio bora kabisa.” (Aya ya 4) Kisha inabainisha kwamba baadhi ya watu wanabaki kwenye Fitra (asili) yao ya mwanzo lakini baadhi ya wengine wanashuka kwenye nafasi ya chini kabisa. “Kisha tukamrudisha kuwa chini kuliko walio chini!” (Aya 5)

Kwa hiyo uumbaji wa mwanadamu unatokana na Fitra ya Mwenyezi Mungu na Ahsan Taqwim (umbo bora zaidi) lakini watu wamegawanyika katika makundi mawili ya waumini na makafiri.

Mungu anaapa kwa vitu vinne ili kusisitiza kwamba mwanadamu ameumbwa kwa njia bora zaidi. Lakini ni juu ya kila mtu kutumia vyema uwezo na uwezo wake ili kufikia hadhi ya juu zaidi na (akhera) kufurahia maisha ya furaha ya milele pamoja na Mungu wake.

Baadhi ya wafasiri wamesema Ahsan Taqwim inahusu umbile lenye nguvu na sawia la mwili katika umri mdogo na Asfal Safilin (chini kuliko walio chini!) inahusu udhaifu wa mwili wakati mtu anazeeka. Aya ya 6 inawatenga Waumini na wafanyao wema wasiingie kwenye Asfal Safilin kwa kusema, “Lakini wale walio amini na wakatenda mema, hao watapata ujira usio kwisha”

Ama kutajwa mtini na zeituni katika Sura hii, kuna mitazamo tofauti baina ya wafasiri. Wafasiri wengi wanasema inahusu misikiti miwili, mmoja katika Sham na mwingine al-Quds au milima miwili inayoitwa Tina na Zita katika maeneo haya mawili.

Kwa mujibu wa baadhi ya watu wengine, maneno hayo mawili yanahusu sehemu ambazo Nabii Isa (AS) alizaliwa na kuishi.

Katika mstari wa 2 na 3 Mwenyezi Mungu anazungumza kuhusu Tur Seeneen na Balad Ameen. Wafasiri wengi wanasema ya kwanza inarejelea Mlima Sinai ambapo Mungu anazungumza na Musa (AS) na ya pili Makka.

Habari zinazohusiana
captcha