Jassem Muhammad al-Budaiwi, Katibu Mkuu wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi amelaani kitendo cha kundi lenye misimamo mikali cha kuvunjia heshima Qur’ani tukufu mbele ya baadhi ya balozi huko Uholanzi na kusema kuwa, vitendo kama hivi ni vya chuki na vya kichochezi.
Kiongozi huyo mwandamizi wa Baraza la Ushirikiano wa Ghuba ya Uajemi ameitaka jamii ya kimataifa kuchukua hatua za haraka na athirifu kwa ajili ya kukabiliana na vitendo kama hivi.
Al-Budaiwi aidha amesema, kwa bahati mbaya, vitendo hivi vimerudiwa tena hivi karibuni kwa kisingizio cha uhuru wa kujieleza na hakuna majibu ya wazi yaliyofuatiwa na vitendo hivi.
Katibu Mkuu wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi pia amesisitiza kuwa, nchi yanazotokea matukio hayo zinapaswa kuchukua hatua mara moja kwa sababu zinawajibika kisheria na kimaadili.
Kwa upande mwingine, Bunge la Kiarabu pia limelaani kitendo cha kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu huko Uholanzi na kusisitiza kwamba, halikubaliani kabisa na vitendo hivyo vya kutowajibika vinavyosababisha chuki na vurugu na kutishia amani na usalama wa kimataifa.
Bunge la Kiarabu limetoa mwito wa kuanzishwa kwa sheria za kimataifa ili kuheshimu matukufu ya dini na kukabiliana na ghasia na itikadi kali.
Bunge hilo limesisitiza kwamba, kung’ang’ania vitendo hivyo visivyo vya kimaadili kunasababisha kuibuka mizozo na mivutano sambamba na kupotea hali ya kuheshimiana watu na mataifa.