IQNA

Mtazamo wa Maadili Katika Qur'ani/ 5

Akhlaqi njema ni Baraka ya Mwenyezi Mungu

20:13 - March 11, 2024
Habari ID: 3478490
IQNA - Akhlaki njema au tabia njema ni muhimu sana na ina athari nyingi chanya katika mahusiano ya watu na katika mwingiliano wa kijamii.

Qur'ani Tukufu inasisitiza umuhimu wake kwa wote na hasa inasisitiza kwamba ni muhimu kwa Mitume wa Mwenyezi Mungu kuwa na uwezo bora wa kuwaongoza watu.

Akhlaqi njema ina fungu kubwa katika kueneza fadhili na kufanya maneno ya mtu yawe na matokeo. Ndiyo maana Mungu, Mwingi wa Rehema, alituma wajumbe na manabii waliokuwa wapole na wenye tabia njema ili waweze kuwavuta watu kwenye ukweli.

Mwenyezi Mungu anasema katika Aya ya 159 ya Surah Al Imran: “Basi ni kwa sababu ya rehema itokayo kwa Mwenyezi Mungu ndio wewe (Muhammad) umekuwa laini kwao. Na lau ungeli kuwa mkali, mwenye moyo mgumu, bila ya shaka wangeli kukimbia. Basi wasamehe, na waombee maghfira, na shauriana nao katika mambo. Na ukisha kata shauri basi mtegemee Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wanao mtegemea."

Mitume wa Mwenyezi Mungu walikuwa wapole na wema na waliwatendea watu kwa tabia njema kiasi kwamba hawakuwavutia tu watafutaji ukweli na kuwaongoza kwenye njia sahihi, lakini pia wakati mwingine waliwafanya maadui wajionee aibu wao wenyewe na tabia zao. Mtume Muhammad (SAW) alikuwa ni mfano bora kabisa wa tabia njema kama hii, kuhusu ambaye Qur'ani Tukufu inasema: “Na hakika wewe una tabia tukufu. (Aya ya 4 ya Surah Al-Qalam)

Kwa hiyo tabia njema ni muhimu sana katika mahusiano ya kibinadamu na ina faida nyingi za kijamii. Inasaidia kuvutia umakini wa watu na mapenzi pamoja na imani yao.

Katika Aya ya 83 ya Surah Al-Baqarah, Mwenyezi Mungu, katika kufanya agano na Bani Isra’il, anasema: “... na semeni na watu kwa wema, na shikeni Sala, na toeni Zaka. Kisha mkageuka isipo kuwa wachache tu katika nyinyi; na nyinyi mnapuuza.

Kwa mujibu wa Aya za 43 na 44 za Surah Taha, kuwa na tabia njema na kuwahurumia watu pia ni muhimu katika kukabiliana na maadui, hasa tunapojaribu kuwaalika kwenye ukweli. Ndiyo maana Musa (AS) anapoamrishwa kufikisha ujumbe wa kimungu kwa Firauni, anaambiwa: “Nendeni kwa Firauni. Hakika yeye amepindukia mipaka. Mwambieni maneno laini, huenda akazingatia au akaogopa.

Kwa hiyo, wakati kukataza maovu na kukaribisha ukweli kunafanywa kwa upole na wema, inatumainiwa kwamba wenye mioyo migumu zaidi wataathiriwa.

3487415

captcha