Wabunge Jumatano walipiga kura ya kuunga mkono mawaziri wote waliopendekezwa na rais baada ya siku tano za vikao na majadiliano.
Mnamo Agosti 11, siku 12 baada ya hafla ya kuapishwa kwake rais Pezeshkian aliwasilisha orodha ya mawaziri bungeni ili kuchunguzwa na kupigiwa kura ya imani
Ikumbukwe kuwa kufuatia ajali mbaya ya helikopta iliyosababisha kifo cha Rais Ebrahim Raisi mnamo Mei 19, Pezeshkian aliibuka kuwa mmoja wa wagombea sita wa mwisho waliochaguliwa na Baraza la Kulinda Katiba kutoka miongoni mwa kundi la watu 80 waliokuwa wamejiandikisha kugombea urais.
Alipata kura nyingi zaidi katika duru ya kwanza ya uchaguzi wa rais mnamo Juni 28 ambapo hakuna mshindi mutlaki aliyepatikana na hivyo na akapambana na mshindi wa pili, Saeed Jalili, katika marudio ya uchaguzi wa Julai 5. Pezeshkian ambaye ni daktari wa moyo alishinda duru ya pili kwa kupata 53.66% ya kura.
Akizungumza Jumapili wakati alipofika bungeni kuteta baraza lake la mawaziri, Rais Pezeshkian alisema: “Baraza la mawaziri lililowasilishwa bungeni leo ni serikali ya umoja wa kitaifa; serikali ya umoja wa kitaifa ni serikali inayojiona kuwa serikali ya watu wote wa Iran. Serikali ya umoja wa kitaifa ina wajibu wa kutetea haki za raia za Wairani wote na imejitolea kuweka kipaumbele kwa maslahi ya kitaifa kuliko maslahi mengine yoyote."
4232565