IQNA

Siasa

Ayatullah Khamenei amuidhinisha rasmi Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Masoud Pezeshkian

20:53 - July 28, 2024
Habari ID: 3479196
IQNA-Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei ameutaja uchaguzi wa Rais wa Awamu ya 14 wa Jamhurii ya Kiislamu ya Iran kuwa ni wa mafanikio ya taifa katika mtihani muhimu. Ameyasema hayo leo mjini Tehran katika sherehe ya amemuidhinisha rasmi Rais wa Awamu ya 14 wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Masoud Pezeshkian.

Ameeleza matumaini yake kuwa matokeo matamu ya uchaguzi huo yatahisiwa na wananchi wa Iran, na kuitaja demokrasia ya sasa nchini kuwa ni zawadi ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Kiislamu kwa taifa na kusimama kidete wananchi dhidi ya hali mbaya iliyokuwa ikitawala. Ayatullah Khamenei amesema: Katika kipindi cha zaidi ya miaka arubaini iliyopita, makumi ya uchaguzi zimefanyika hapa nchini zikiandamana na ushindani, usahihi na ushiriki wa watu kwa ari.

Ayatullah Khamenei ametaja hatua za kiuchumi katika masuala makubwa kama vile thamani ya sarafu ya taifa, uzalishaji, uwekezaji, uboreshaji wa mazingira ya biashara na hatua za dharura na za muda mfupi za kuboresha maisha ya watu kuwa ndio mambo ya dharura, na amewatolea wito maafisa na watendaji wa nchi kuthamini na kutegemea uwezo wa ndani.

Amesema serikali iliyopita ilifanya kazi muhimu ambazo zinapaswa kuendelezwa na kupanuliwa zaidi.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, haijuzu kughafilika na matukio ya eneo la Magharibi mwa Asia na  dunia kwa ujumla na kuongeza kuwa: Elezeni waziwazi na kwa uimara msimamo wa nchi kuhusiana na matukio yote ili walimwengu wajue msimamo wa Iran ya Kiislamu.

Ayatullah Khamenei, sanjari na kuashiria vipaumbele vya siasa za nje za nchi, amezungumzia nafasi nzuri ya Iran ya kuwa na majirani wengi na kusisitiza umuhimu wa kufanyakazi kwa bidii kwa ajili ya kuimarisha uhusiano na majirani. Amesema: Kipaumbele kingine cha siasa za nje ni kuwa na uhusiano na nchi kama vile za Afrika na Asia ambako kunaweza kupanua uwanja wa kidiplomasia wa Iran.

Katika sehemu ya mwisho ya hotuba yake, Ayatullah Ali Khamenei amelitaja suala la Gaza kuwa ni kadhia ya kimataifa na kuongeza kuwa: Palestina ilikuwa suala la nchi za Ulimwengu wa Kiislamu tu, lakini hii leo ni suala la watu wote na la kimataifa, na limeingia katika Congress ya Marekani, Umoja wa Mataifa, Olimpiki na medani zote.

Amezungumzia pia suala la kuimarika na kuongezeka nguvu za Muqawama na kusema: "Licha ya misaada yote ya Marekani na baadhi ya nchi za kisaliti, Wazayuni wameshindwa kuzima nguvu ya Muqawama, na lengo lao la kuiangamiza Hamas limefeli; sasa Hamas, Jihadi Islami na makundi mengine ya Muqawama yanaendelea kusimama imara na kwa nguvu zote."

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameitaja hatua ya Bunge la Marekani siku mbili zilizopita ya kumwalika na kumpa ukumbi mhalifu wa vita, Benjamin Netanyahu, kuwa ni fedheha kubwa na kusema: Dunia inapaswa kuchukua uamuzi mzito kuhusiana na Gaza; na serikali, mataifa na shakhsia wa kisiasa na wasomi wanapaswa kuchukua hatua katika nyanja tofauti.

3489264

 

Habari zinazohusiana
captcha