"Qur’ani Tukufu yawataka waislamu kuungana kama jumuiya moja" –Rais Pezeshkian
Mashhad, Iran – "Qur’ani inawataka Waislamu waungane kama jamii moja na washikilie kwa nguvu kamba ya Mwenyezi Mungu ili kuepuka mgawanyiko," aliandika Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, katika ujumbe wake uliosomwa wakati wa sherehe ya kufunga Mashindano ya 41 ya Kimataifa ya Qur’ani mjini Mashhad siku ya Ijumaa.
"Bila shaka, changamoto nyingi zinazoukabili ulimwengu wa Kiislamu leo zinatokana na kupuuzia mafundisho haya, hali inayosababisha mgawanyiko na kufungua njia kwa maadui kutumia migawanyiko hiyo kwa manufaa yao," aliongeza.
Tuzo za Washindi wa Mashindano ya 41 ya Kimataifa ya Qur’ani
Rais Pezeshkian alisisitiza kuwa Qur’an inapita mipaka ya rangi, tabaka, na madhehebu, ikielekeza wanadamu katika ukamilifu wa maadili na roho. "Katika machafuko ya dunia ya leo, Qur’an inatoa msingi imara wa matumaini, ikielekeza njia ya ukombozi kutoka kwa ujinga, dhuluma, na ukosefu wa usawa," alisema.
Pia alionya juu ya juhudi za kimataifa za kupotosha sura halisi ya Uislamu. "Ubeberu wa kimataifa unatumia majukwaa mbalimbali ya vyombo vya habari kueneza hofu dhidi ya Uislamu (Islamophobia) na kuonyesha Qur’an kama tishio kwa ubinadamu," alisema. "Hata hivyo, kwa juhudi za wanazuoni wa Qur’an na wasomaji wake—ambao ni wajumbe wa mafundisho yake duniani kote—njama hizi zitashindwa."
Rais wa Iran aliwashukuru washiriki na waandaaji wa mashindano hayo ya kimataifa, akiwataja kama wahamasishaji wakuu wa ujumbe wa Qur’ani wa umoja na maelewano.
Mashindano ya 41 ya Kimataifa ya Qur’an Yamalizika kwa Mafanikio
Mashindano haya yaliyohitimishwa Ijumaa yalikusanya wasomaji wa kiume na wa kike 57 kutoka nchi 27 katika jiji la Mashhad, kaskazini mashariki mwa Iran. Tukio hili, mojawapo ya mashindano ya zamani zaidi ya Quran katika ulimwengu wa Kiislamu, lilijumuisha mashindano ya usomaji (qiraa) na hifdh (hifdhu Qur’an).
Taasisi ya Awqaf ya Iran pia ilieleza nia yake ya kuandaa mashindano yajayo ya Kimataifa ya Qur’an katika jiji hilo la Mashhad.
Rais Pezeshkian alihimiza juhudi za kutumia mafundisho ya Qur’ani kuimarisha mazungumzo na mahusiano ya karibu kati ya mataifa.
https://iqna.ir/en/news/3491680/