Jamiu Amau Saliou alihutubia jukwaa la wataalamu lililoitwa “Maisha ya Binadamu: Kuelewa Marufuku ya Kuua Kinyume cha Haki na Uzito wa Mauaji katika Uislamu (Surah Al-Ma’idah, Aya ya 32)”.
Ameyasema hayo katika Kitengo cha Kimataifa cha Maonyesho ya 32 ya Kimataifa ya Qur’ani Tukufu ya Tehran Jumapili jioni.
Saliou alisema kuwa kwa mujibu wa Uislamu, kuua kinyume cha haki hakuruhusiwi tu bali pia linachukuliwa kuwa kitendo kisichokubalika kabisa na kisichosameheka.
Alisema mojawapo ya mada kuu za Qur’ani ni utakatifu wa maisha ya binadamu, na kwa msingi huu, uhifadhi wa maisha ya binadamu unashikilia umuhimu maalum katika Uislamu.
Alibainisha aya mbalimbali za Qur’ani, hasa Aya ya 32 ya Surah Al-Ma’idah, na kusema kwamba Qur’ani inalinganisha kuua kinyume cha haki na kuua wanadamu wote na inaonyesha kuokoa maisha ya mtu mmoja kama kuokoa wanadamu wote.
Alisisitiza heshima ya binadamu na jukumu la watu binafsi kulinda maisha, akisema kuwa binadamu, kama wawakilishi wa Mungu duniani, wana jukumu la kudumisha haki na kuzuia mauaji kinyume cha haki.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Saliou alichambua maoni ya wafasiri maarufu wa Qur’ani kuhusu mauaji kinyume cha haki na kueleza kwamba kwa mujibu wao, Aya ya 32 ya Surah Al-Ma’idah inatumika kama kanuni ya kimaadili ya ulimwengu, sio tu kwa Waislamu bali kwa wanadamu wote.
Pia alijadili idhini ya kuua, akibainisha kwamba katika hali maalum, kama vile Qisas (kisasi) au kuadhibu mwenye kueneza ufisadi duniani, kuchukua maisha ya mtu ni halali.
Hata hivyo, hapa sharia hii inatumika tu katika mazingira maalum na lazima kuwa na msingi wa kisheria katika utekeleza adhabu, alisema.
Saliou alirejelea maoni ya wafasiri wa Qur’ani kama Allamah Tabatabaei, Sheikh Tousi, al-Tabari, na Ibn Kathir, akisema aya hii imewasilishwa kama kanuni ya maadili ya ulimwengu, hasa inatumika katika tamaduni mbalimbali za binadamu.
Alibainisha kwamba baadhi ya wafasiri wanasisitiza umuhimu mkubwa wa kuhifadhi maisha ya binadamu katika Qur’an na mafundisho ya Kiislamu.
Maonyesho ya 32 ya Kimataifa ya Quran Tukufu ya Tehran yanaendelea katika ukumbi wa Mosalla Imam Khomeini (RA) na yalianza Machi 5 na yataendelea hadi Machi 16, 2025.
Maonyesho ya mwaka huu yana programu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na vipindi maalum, warsha za kielimu, mikutano ya Qur’ani, na shughuli maalum kwa watoto na vijana.
Maonyesho hayo hufanyika kila mwaka katika mwezi mtukufu wa Ramadhani na Wizara ya Utamaduni na Mwongozo wa Kiislamu ya Iran.
Lengo lake ni kukuza fikra za Qur’ani na kuendeleza shughuli za Qur’ani.
Maonyesho hayo pia ni jukwaa la mafanikio ya hivi karibuni katika sekta ya Qur’ani nchini Iran.
3492257