IQNA

Maonyesho ya 32 ya Kimataifa ya Qur'ani Tehran Kutilia Mkazo Ushiriki wa Familia na Vijana

9:44 - March 04, 2025
Habari ID: 3480303
IQNA – Maonyesho ya 32 ya Kimataifa ya Qur'ani jijini Tehran yataangazia ushiriki wa familia na vijana, yakionyesha mafanikio ya Qur'ani nchini Iran, amebaini mkuu wa tukio hilo.

Mkutano wa waandishi wa habari kwa ajili ya Maonyesho ya 32 ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu ulifanyika Machi 3 katika Idara ya Qur'ani na Etrat ya Wizara ya Utamaduni na Mwongozo wa Kiislamu.

Kikao hicho kilihudhuriwa na Hujjatul Islam Hamidreza Erbab-Soleimani, mkurugenzi wa maonyesho na Naibu wa Waziri wa Masuala ya Qur'ani na Etrat katika Wizara ya Utamaduni na Mwongozo wa Kiislamu ya Iran, pamoja na Asghar Amirnia, katibu wa baraza la upangaji wa maonyesho hayo.

"Qur'ani ni kitabu cha mwongozo, si hadithi tu. Ingawa ina masimulizi, lengo lake kuu ni kuwaongoza wenye taqwa," alisema Erbab-Soleimani. "Ni chanzo cha nuru, baraka, uwazi, na ubainishaji."

Pia alielezea uhusiano kati ya Ramadhani na Qur'ani. "Ramadhani ni mwezi ambao Qur'ani iliteremshwa. Hili linaongeza umuhimu wa mwezi huu, na hata utukufu wa Laylatul-Qadr unahusiana na kushushwa kwa Qur'ani."

Wizara ya Utamaduni na Mwongozo wa Kiislamu inaandaa maonyesho haya kwa heshima ya Ramadhani. "Lengo letu kuu ni kuonyesha mafanikio na uwezo wa Qur'ani nchini Iran," alisisitiza Erbab-Soleimani.

Maonyesho ya 32 ya Kimataifa ya Qur'ani yatafanyika kuanzia Machi 5 hadi Machi 16 katika Ukumbi wa Msikiti wa Mosalla jijini Tehran. Muda wa kutembelea ni saa kumi jioni hadi tano usiku kwa siku za kawaida na saa nane mchana hadi tano usiku kwa siku za mapumziko. Kaulimbiu ya mwaka huu ni “Qur’ani; Njia ya Maisha.”

"Mwaka huu, maonyesho yanazingatia zaidi familia na vijana," aliongeza Erbab-Soleimani.

Alibainisha kuwa tukio hilo linachukua eneo la mita za mraba 20,000 na lina sehemu 37, ambapo 27 kati ya hizo zinaendeshwa na taasisi kuu za umma.

Mashirika 15 ya serikali na yasiyo ya serikali yatashiriki, pamoja na taasisi 40 za umma, huku zaidi ya wachapishaji 120 wakionesha zaidi ya vitabu 4,000 vinavyohusiana na Qur'ani Tukufu

Tukio hilo pia litahusisha uzinduzi wa kazi mpya tisa zinazohusiana na Qur'ani na Ahlul-Bayt (AS), pamoja na mijadala 58 ya kitaalamu na mikutano 26 ya Qur'ani.

"Tumepokea uthibitisho kutoka kwa nchi 15 zinazoonyesha nia ya kuwasilisha kazi zao za Qur'ani katika maonyesho haya," alisema Erbab-Soleimani.

Hafla maalum ya kuwaenzi wanazuoni wa Qur'ani na wachangiaji wa masuala ya Qur'ani itafanyika mwishoni mwa maonyesho. "Hili ni jadi yetu ya kila mwaka, na mwaka huu, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran atahudhuria hafla ya kufunga tukio," aliongeza.

Akijibu swali kuhusu maendeleo ya kiteknolojia, Erbab-Soleimani alithibitisha kuwa zana za kisasa, zikiwemo Akili Mnemba (AI) na uhalisia ulioboreshwa (AR), zitaingizwa katika maonyesho haya. "Tumeandaa sehemu maalum kwa ajili ya AI," alitangaza.

Pia alieleza kuwa kutakuwa na uzinduzi wa kila siku wa kazi mpya za Qur'ani, ikiwemo tafsiri ya Qur'ani kwa Kihindi na tafsiri ya Qur'ani iliyoandikwa na Ayatullah Javadi Amoli.

Asghar Amirnia, katibu wa baraza la upangaji, alisisitiza mvuto mpana wa maonyesho hayo. "Tumebuni sehemu zinazokidhi mahitaji mbalimbali, ikiwemo kimataifa, kisanii, familia, watoto, pamoja na unyenyekevu na hijabu," alisema.

Kuhusu huduma kwa umma, Amirnia alisema kuwa mipango imefanywa kwa kushirikiana na manispaa ili kutoa futari rahisi kwa wageni, kama ilivyokuwa miaka iliyopita.

Picha rasmi ya maonyesho haya inaonesha aya ya 97 kutoka Surah An-Nahl:

" Mwenye kutenda mema, mwanamume au mwanamke, naye akawa ni Muumini, tutamhuisha maisha mema; na tutawapa ujira wao kwa bora ya waliyo kuwa wakiyatenda."

Hafla ya ufunguzi wa maonyesho haya imepangwa kufanyika Jumatano saa tisa alasiri kwa saa za Tehran.

4269426

Habari zinazohusiana
captcha