IQNA

Dua ya Gaza na Al-Aqsa katika Masjid Al Haram wakati wa Swala ya Ijumaa

14:33 - March 29, 2025
Habari ID: 3480464
IQNA- Swala ya Ijumaa ya mwisho wa mwezi mtukufu wa Ramadhani katika misikiti mbalimbali duniani, ikiwemo Msikiti wa Masjid al Al-Haram katika mji mtakatifu wa Makka, na Msikiti wa Al-Azhar nchini, iliandamana na dua kwa ajili ya Wapalestina wa Gaza na Msikiti wa Al-Aqsa.

Kulingana na ripoti, dua kwa Wapalestina wa Ukanda wa Gaza ilikuwa katika mstari wa mbele wa dua za swala ya Ijumaa ya mwisho wa mwezi mtukufu wa Ramadhani, na wito wa dua hii ulitangazwa tangu mwanzoni mwa mwezi Machi mwaka huu katika baadhi ya misikiti ya ulimwengu wa Kiarabu na Kiislamu, hasa misikiti muhimu kama vile Masjid al-Haram Msikiti wa Al-Azhar na pia Msikiti wa Sultan Hasan nchini Misri.

Sheikh Yasser Al-Dosari, khatibu wa Masjid al Al-Haram, jana katika khutba za swala ya Ijumaa aliomba dua kwa ajili ya Msikiti wa Al-Aqsa akisema: "Mola! Linda Msikiti wa Al-Aqsa na uufanye uwe na heshima na hadhi mpaka Siku ya Kiyama."

Khatibu wa Msikiti wa Al-Azhar pia katika khutba za swala ya Ijumaa aliomba dua kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili Wapalestina katika Gaza na kuondoa njama za maadui.

Khatibu wa Msikiti wa Sultan Hasan katika eneo la kihistoria la Cairo, mji mkuu wa Misri, pia alimuomba Mwenyezi Mungu awalinde watu wa Gaza na awape ushindi wao dhidi ya maadui.

Israel tangu tarehe 7 Oktoba 2023, kwa msaada kamili wa Marekani, imefanya mauaji ya kimbari katika Gaza na kuua zaidi ya Wapalestina 50,000 na kuwajeruhi wengine zaidi ya 110,000. Wanawake na Watoto ndio waliouawa kwa wingi katika mashambulizi hayo. Aidha katika vita hivi vya kikatili, zaidi ya Wapalestina 14,000 wametoweka na imaaminika walipoteza maisha na bado wako katika vifusi.

4274177

Kishikizo: gaza palestina
captcha