IQNA

Mwanazuoni asisitiza mazungumzo ya nchi za Kiislamu ili kutatua changamoto za ubinadamu

23:10 - May 15, 2025
Habari ID: 3480688
IQNA- Mkuu wa Shirika la Iran la Utamaduni na Mahusiano ya Kiislamu (ICRO) amesema kuwa mazungumzo kati ya nchi za Kiislamu ni hitaji lisiloweza kuepukika katika kutatua changamoto za msingi za ubinadamu.

Hujattul Islam Mohammad Mehdi Imanipour alitoa kauli hiyo wakati akihutubia mkutano wa mawaziri wa utamaduni wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC), uliofanyika Kazan, katika Jamhuri ya Tatarstan nchini Russia, siku ya Alhamisi.

Amehimiza umuhimu wa kuimarisha mazungumzo ya kitamaduni na kuanzisha taasisi madhubuti za kushughulikia changamoto za kimataifa.

Mwanazuoni huyo alieleza furaha yake kwa kukutana na maafisa wa ngazi za juu kutoka nchi za Kiislamu na kusifu uteuzi wa mada ya kikao hiki, akisema, "Leo, zaidi ya wakati mwingine wowote, tunahitaji mazungumzo ya kujenga kati ya serikali na mataifa, hasa nchi za Kiislamu."

Akirejelea mabadiliko ya haraka ulimwenguni, alisema kuwa katika kipindi hiki cha mageuzi ya kihistoria, ni lazima kufanyika mazungumzo ya mara kwa mara na jumuishi ili kujadili masuala ya msingi kama haki za binadamu, utawala bora, elimu kwa vijana, mtindo wa maisha, familia, mustakabali wa ustaarabu wa binadamu, na teknolojia mpya, ikiwemo akili bandia.

HujjatulIslam Imanipour pia alikosoa kutofanya kazi kwa taasisi za kimataifa katika kushughulikia migogoro inayoendelea, hususan hali ya watu waliodhulumiwa wa Gaza, akiongeza kuwa "Kutofanya lolote kwa taasisi hizi mbele ya mauaji ya kimbari na dhuluma ya wazi Palestina kumeongeza mateso na hasira ya watu wanaopenda uhuru. Ni muhimu sana kwa OIC kuwa na mchango mkubwa katika kutatua suala la Palestina kama suala la kwanza la ulimwengu wa Kiislamu."

Akimulika haja ya kuunda ushirikiano mpya miongoni mwa nchi za Kiislamu, alisema kuwa suluhisho la tatizo la Palestina linategemea ushirikiano wa nchi za Kiislamu na hatua za pamoja.

Uundaji wa Umma wa Kiislamu ulio na mshikamano ndio njia pekee ya kukabiliana na mfumo wa uhusiano wa kimataifa wa upande mmoja, alisisitiza.

Alimalizia kwa kushukuru serikali ya Shirikisho la Russia, hususan Wizara ya Utamaduni na mamlaka za jiji la Kazan kwa ukarimu wao, akielezea matumaini kwamba maendeleo ya mazungumzo ya kitamaduni yataweka njia wazi kwa mustakabali wa ulimwengu wa Kiislamu.

Mkutano wa 14 wa mawaziri wa utamaduni wa nchi wanachama wa OIC unafanyika Kazan kwa mada "Mazungumzo ya Tamaduni - Msingi wa Kuhifadhi Utambulisho na Utofauti katika Ulimwengu wa Pande Kadhaa".

Kazan, mji mkuu wa Jamhuri ya Tatarstan nchini Russia, umetangazwa kuwa Mji Mkuu wa Utamaduni wa Ulimwengu wa Kiislamu kwa mwaka 2025.

3493102

captcha