IQNA

"Chanzo cha Fahari": Ayatullah Sistani asifia Tafsiri ya Tasnim

17:03 - May 13, 2025
Habari ID: 3480681
IQNA – Ayatullah Ali al-Sistani, kiongozi mashuhuri wa kidini wa madhehebu ya Shia nchini Iraq, amesifu tafsiri ya Qur'ani ya Tasnim iliyoandikwa na msomi wa Kiirani, Ayatullah Abdollah Javadi Amoli, akiitaja kuwa “chanzo cha fahari kwa Waislamu wa madhehebu ya Shia.”

Alitoa kauli hiyo Jumatatu alipokutana na Ayatullah Javadi Amoli huko Najaf. Kwa mujibu wa taarifa kutoka tovuti rasmi ya Ayatullah Sistani, wanazuoni hao wawili walijadili masuala mbalimbali kuhusu elimu za Kiislamu, maadili, na hali ya Ulimwengu wa Kiislamu kwa ujumla katika mazingira ya kirafiki na kielimu.

Akimkaribisha mgeni wake, Ayatullah Sistani alionyesha kuthamini juhudi za kisomi zilizowekwa kwenye tafsiri hiyo ya Tasnim kwa miongo kadhaa, akisema: “Umeishi na Qur'ani Tukufu kwa miaka 40 na umefanya kazi kwa bidii. Kazi hii ni chanzo cha fahari kwa Uislamu wa Kishia.”

Tafsiri ya Tasnim inachukuliwa kuwa miongoni mwa tafsiri za kisasa na pana zaidi za Qur'ani katika Ulimwengu wa Kiislamu. Ikiwa na juzuu 80, inachanganya mbinu za kale na za kisasa, ikichota kutoka katika taaluma za lugha, falsafa, teolojia na tasawwuf. Inafuata mbinu ya kufasiri “Qurani kwa Qurani,” ambapo kila aya huchambuliwa katika hatua nne: ufafanuzi kwa muhtasari, tafsiri ya kina, tafakuri na uchambuzi kwa mujibu wa Hadithi.

Ayatullah Sistani pia alisisitiza nafasi ya msingi ya Qur'ani katika fikra za Kiislamu, akisema: “Qur'ani ndio msingi. Riwaya za Ahl al-Bayt (AS) lazima zipimwe kwa mtazamo Qur'ani, na zile tu zinazolingana nayo ndizo za kuaminika.”

Aliongeza kuwa hakuna tofauti katika mtazamo wake kati ya Hauza au vyuo vikuu vya Kiislamu vya Qom na Najaf, na akaeleza dhamira yake ya kusaidia taasisi za kidini kwa kadiri awezavyo.

Kwa upande wake, Ayatullah Javadi Amoli alimtaja Ayatullah Sistani kuwa ni nguzo muhimu ya urithi wa kielimu wa Shia na kiongozi mwenye huruma kwa jamii ya wanazuoni na kwa watu wa Iraq. Aliongeza kuwa mwongozo wa Ayatullah Sistani wakati wa nyakati nyeti—hasa alipokabiliana na makundi yenye misimamo mikali kama Daesh—umeacha athari ya kudumu.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya vyuo vya kidini vya nchi mbalimbali na akaeleza shukrani zake kwa msaada endelevu wa Ayatullah Sistani katika elimu ya Kiislamu.

3493070

captcha