IQNA

Watetezi wa Qur'ani Tukufu

Al Azhar: Kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu kuwe kichocheo cha kuimarisha umoja wa Waislamu

17:04 - August 01, 2023
Habari ID: 3477367
TEHRAN (IQNA)- Sheikh wa Al-Azhar wa nchini Misri, akijibu barua ya mkuu wa vyuo vya kidini vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ameeleza matumaini yake kuwa msimamo wa pamoja uliochukuliwa na Waislamu hivi karibuni katika kukabiliana na suala la kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu utakuwa kichocheo cha kutatua tofauti na kuleta umoja baina yao.

Ahmed al-Tayyib Sheikh Mkuu wa al-Azhar ya Misri amesema katika taarifa kwamba amepokea barua ya Ayatullah Alireza Arafi, Mkuu wa Vyuo vya Kidini katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu suala hilo, kwa moyo mkunjufu na furaha kubwa.

Baada ya vitendo vya kuidhalilisha Quran Tukufu katika nchi za Ulaya na hasa nchini Sweden na Denmark, Ayatollah Arafi alimwandikia barua Sheikh Mkuu wa al-Azhar, akimshukuru kwa msimamo wake, na kutaka nchi za Kiislamu zichukuwe hatua kali dhidi ya nchi mbili hizo.

Kwa mujibu wa gazeti la Misri la al-Ahram, Sheikh wa al-Azhar ameeleza matumaini yake kwamba tukio hilo la kinyama na lisilo la kiustaarabu litakuwa kichocheo cha kutatuliwa tofauti zilizopo kati ya Waislamu wa Mashariki na Magharibi na kuimarisha umoja wao katika kukabiliana na changamoto zinazotishia usalama na matukufu yao.

Sheikh wa al-Azhar pia amesisitiza azma yake ya kuandaa mazingira ya kufanyika midahalo ya Kiislamu baina ya wanazuoni wa Kiislamu duniani kote bila ya kujali tofauti zao za kimadhehebu na kimirengo kwa lengo la kuimarisha umoja na maelewano miongoni mwao na kuepuka fitina na hitilafu.

Al-Azhar imeongeza kuwa, itaendelea kutekeleza jukumu lake la kuunga mkono dini ya Kiislamu na kukabiliana na udhalilishaji wowote dhidi yake, na kwamba iko macho kupambana na wale wanaokusudia kuwavunjia heshima Waislamu na matukufu yao.

Sheikh wa al-Azhar pia ametoa wito kwa mataifa yote ya Kiarabu na Kiislamu kuendeleza marufuku ya bidhaa za Uswidi na Denmark kwa ajili ya kutetea Quran Tukufu.

Hivi karibuni, raia mmoja wa Uswidi kwa jina la Salvan Momika, alichoma moto nakala ya Qur'ani Tukufu huko Stockholm, mji mkuu wa nchi hiyo, kitendo cha kuchukiza ambacho kiliibua hasira na malalamiko makali ya nchi za Kiislamu.

3484593

Habari zinazohusiana
captcha