Profesa Laleh Eftekhari wa Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Azad nchini Iran alitoa kauli hiyo katika semina ya mtandaoni iliyofanyika Jumanne, yenye kichwa: “Lugha ya Muujiza wa Qur’ani: Tathmini ya Kitabu cha Bassam Saeh.”
Profesa Eftekhari alisema kuwa kuanzia karne ya 11 hadi katikati ya karne ya 20, mustashriqin (wataalamu wa Ulaya wanaofanya utafiti kuhusu Uislamu) “kwa kujua au bila kujua, walitoa mitazamo ya uadui na kuweka tafsiri zao.” Hata hivyo, aliongeza: “Mchango wao ni kwamba walitulazimisha kuitetea Qur’ani, kuisoma, kuandika, na kuithamini zaidi uzuri wake.”
Aliendelea kusema: “Utoaji wa mitazamo ya uadui ni ushahidi wenyewe wa muujiza wa Qur’ani, kwa sababu maadui wa Qur’ani hawajaweza kuleta kilicho kama hicho. Hili limefungua milango mipya ya utafiti wa kina.”
Eftekhari alikanusha madai kuwa lugha ya Qur’ani ni Kisiria ( Syriac) , akitaja hoja hizo kuwa “hazina msingi.” Akikinukuu Qur’ani, alisema: “Hatukumtuma mtume yeyote ila kwa lugha ya watu wake, ili awafafanulie wazi ujumbe wa Mwenyezi Mungu” [Qur’ani 14:4].
Aliongeza: “Licha ya kupita kwa karne kumi na nne, hakuna aliyeweza kuwasilisha hoja ya kisayansi au ya kiakili inayopingana na Qur’ani.”
Kwa mujibu wake: “Lugha ya Qur’ani ni lugha ya watu wake. Tafsiri husaidia wale ambao si walengwa wa awali kuielewa.”
Alielezea changamoto ya Qur’ani (tahaddi) kuwa ya kimataifa, akibainisha kuwa tofauti na vitabu vingine vya mbinguni, “Mwenyezi Mungu ameihakikishia Qur’ani kuhifadhiwa, na hivyo kuwa muujiza wa milele.”
Akikumbuka simulizi la mapema ya Kiislamu, alisema kundi la washairi Waarabu walijaribu kuishindana na Qur’ani. “Walimtuma Walid kukutana na Mtume, lakini alipo rudi alisema: ‘Hii ni hotuba inayozidi zote; si maneno ya mwanadamu.’”
Eftekhari alisisitiza ufasaha wa Qur’ani na usahihi wa lugha yake kuwa ushahidi wa kudumu wa upekee wake. “Kurudiarudia kwa viapo mwanzoni mwa aya huvutia umakini; lahani yake haina mfano; hakuna neno linaloweza kubadilishwa,” alisema.

Aliongeza kuwa vipengele vingine vya muujiza wa Qur’ani ni pamoja na utabiri wa matukio ya baadaye na maarifa ya kisayansi. “Qur’ani ilielezea hatua za ukuaji wa kiinitete cha binadamu miaka 1,400 iliyopita, wakati hakuna zana za kisayansi kama ultrasound,” alisema. “Ni muujiza wa kisayansi katika nyanja nyingi, unaompa kila mtu fursa ya kunufaika kulingana na uwezo wake.”
Profesa Eftekhari alibainisha kuwa kuelewa tabaka mbalimbali za lugha ya Qur’ani kunahitaji utafiti wa taaluma mbalimbali unaochanganya masomo ya Qur’ani na sayansi za kisasa.
“Sisi si wa kuwalazimisha watu waongoke,” alisema, “lakini tunawajibika kufikisha ukweli ili watu wasipotee. Qur’ani ndiyo chanzo bora cha ujumbe huu.”
Alisisitiza: “Kadri sayansi inavyoendelea, ndivyo ukweli na muujiza wa Qur’ani unavyozidi kuwa wazi. Changamoto ya Qur’ani itaendelea kuwa hai katika nyakati na maeneo yote.”
3495101