IQNA

Ayatullah Khamenei amtaja Allamah Naeini kuwa Nguzo ya Kielimu katika Chuo cha Kale cha Najaf

14:48 - October 24, 2025
Habari ID: 3481408
IQNA – Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, amemtaja Allamah Mirza Muhammad Hussain Naeini (Rehmatullah alayh) kama mmoja wa nguzo mashuhuri zaidi za kielimu na kiroho katika Hawza (Chuo kikuu cha Kiislamu) ya kale ya Najaf, Iraq.

Kauli hizo za Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu zilitolewa Alhamisi asubuhi wakati wa hafla ya kimataifa ya kumbukumbu ya Allamah Naeini iliyofanyika mjini Qom, ambapo hotuba yake iliyotolewa katika kikao na waandaaji wa tukio hilo siku ya Jumatano, Oktoba 22, ilisomwa rasmi.

Katika kikao hicho, Ayatullah Khamenei alimsifu Allamah Naeini kama msomi wa kiwango cha juu ambaye mchango wake uliimarisha msingi wa kielimu na kiroho wa chuo hicho cha kale cha Najaf.

Akiangazia kipengele cha kitaaluma cha Allamah Naeini, Kiongozi Muadhamu alisema kwamba sifa yake kuu ilikuwa jinsi alivyounda mfumo wa ufundishaji katika elimu ya misingi ya fiqhi (Usul al-Fiqh). Mfumo huo, alisema, ulijengwa juu ya utaratibu wa kiakili na kisayansi, na uliheshimiwa kwa ubunifu wake thabiti na wa hali ya juu.

Ayatulah Khamenei pia alisisitiza kipaji kingine adhimu cha Allamah Naeini — fikra zake za kisiasa. Fikra hizo, alieleza, zimebainishwa katika kitabu chake muhimu chenye umaarufu mdogo, “Tanbih al-Ummah” (Uelekezi wa Ummah).

Kiongozi Muadhamu alieleza kwamba misingi ya fikra za kisiasa za Allamah Naeini inategemea dhana ya kusimamisha serikali ya Kiislamu inayozingatia uongozi wa kimungu (Wilayah), kama mbadala wa utawala wa kidhalimu. Aidha, alisisitiza kuwa kwa mujibu wa maono ya Allamah Naeini, serikali na viongozi wake wote lazima wawe chini ya uwajibikaji na usimamizi wa wananchi.

Hivyo, alisema, kunahitajika kuundwa kwa baraza la wawakilishi wa wananchi kupitia uchaguzi, ambalo litakuwa na jukumu la kutunga sheria na kusimamia serikali, huku uhalali wa sheria hizo ukitegemea idhini ya maulamaa na wanazuoni mashuhuri wa Kiislamu.

Ayatullah Khamenei alifafanua kwamba mfumo wa serikali ulioelezwa na Allamah Naeini — unaochanganya Uislamu na utawala wa wananchi — leo unaweza kueleweka kama “Jamhuri ya Kiislamu.”

Akizungumzia sababu iliyomfanya Allameh Naeini mwenyewe kukusanya maandiko ya kitabu chake Tanbih al-Ummah, Kiongozi wa Mapinduzi alisema kuwa Harakati ya Kikatiba (Constitutional Movement) nchini Iran iliyoungwa mkono na Allamah Naeini na wanazuoni wa Najaf, kimsingi ilikuwa juhudi ya kusimamisha serikali ya haki na kumaliza udhalimu.

Alibainisha kuwa harakati hiyo ilikuwa tofauti kabisa na ile katiba bandia iliyoundwa na Waingereza nchini Iran, ambayo ilisababisha migogoro na matokeo mabaya kama kuuawa kwa Sheikh Fazlollah Nouri.

Katika kikao hicho, Ayatullah Alireza Arafi, Mkurugenzi wa Vyuo vya Dini (Hawza), aliwasilisha ripoti kuhusu maandalizi, programu na shughuli mbalimbali za maadhimisho ya kimataifa ya kumkumbuka Allamah Naeini.

Chanzo: Khamenei.ir

3495123

Habari zinazohusiana
Kishikizo: ayatullah khamenei
captcha