IQNA

Kituo cha Al-Azhar Chatoa Onyo Kuhusu Matumizi Mabaya ya Akili Mnemba Kusambaza Chuki Dhidi ya Waislamu nchini India

17:18 - October 21, 2025
Habari ID: 3481391
IQNA – Kituo cha Al-Azhar cha Kupambana na Itikadi Kali kimetoa onyo kali kuhusu matumizi mabaya ya teknolojia ya Akili Mnemba (AI) katika kuchochea chuki dhidi ya Waislamu nchini India.

Taarifa hiyo imetolewa kufuatia video iliyosambazwa na chama cha Bharatiya Janata Party (BJP) katika jimbo la Assam, ambayo inadaiwa kutumia zana za AI kutengeneza maudhui ya chaguzi yenye chuki dhidi ya Uislamu. Video hiyo ilichapishwa katika akaunti rasmi ya chama hicho kwenye mtandao wa X (zamani Twitter) mnamo tarehe 15 Septemba 2025.

Kwa mujibu wa kituo hicho, video hiyo “inaonesha taswira potofu ya Waislamu kama ‘tishio la idadi ya watu’ na inakuza madai hatari yanayolenga kueneza hofu na chuki katika jamii.”

Taarifa hiyo imeongeza kuwa ujumbe kama huo ni “aina ya wazi ya chuki dhidi ya Uislamu na hotuba ya chuki inayopingana na maadili ya kibinadamu na Katiba inayojengwa juu ya misingi ya uraia na haki.”

Kituo hicho pia kimeonya kuwa matumizi ya akili bandia kutengeneza propaganda za kisiasa “yanatengeneza mfano hatari kwa kampeni za uchaguzi na yanahatarisha kwa kiwango kikubwa amani ya kiraia na maelewano ya kidini.”

Al-Azhar imetoa wito kwa Tume ya Uchaguzi ya India kuanzisha uchunguzi wa haraka kuhusu uhalali wa video hiyo. Aidha, imehimiza mamlaka husika kuandaa kanuni madhubuti za kidijitali kuhusu matumizi ya AI katika kampeni za kisiasa, na kuimarisha usimamizi wa majukwaa ya mtandaoni ili kupunguza ueneaji wa hotuba za chuki.

Kituo hicho kimesisitiza kuwa teknolojia za kisasa zinapaswa “kuhudumia ubinadamu, maendeleo, na kuendeleza amani ya kijamii – si kuwa nyenzo za mgawanyiko na uchochezi.”

3495074

captcha