IQNA

Kongamano la Kwanza la Kimataifa la “Qur’an ya Negel” Lafanyika Sanandaj

17:34 - October 21, 2025
Habari ID: 3481394
IQNA – Kongamano la kwanza la kimataifa la “Qur’an ya Negel” limefanyika mjini Sanandaj siku ya Jumatatu, likiwakutanisha makari na wahifadhi wa Qur’an wanaozungumza Kikurdi kutoka Iran, Uturuki na Iraq.

Tukio hilo limefanyika katika ukumbi wa Fajr na kuendelea hadi sala za Magharibi na Isha. Liliandaliwa sambamba na Mashindano ya Kitaifa ya Qur’ani ya Iran ya 48, ambayo mwaka huu yanafanyika katika mkoa wa Kordestan.

Kongamano hili limepewa jina la Qur’ani maarufu ya mkono ya kijiji cha Negel, kilichoko katika mkoa wa Kordestan, ambacho kinajulikana kwa kuhifadhi nakala ya kale ya maandishi ya Kufi yaliyoandikwa juu ya ngozi ya paa.

Nakala hiyo, ambayo inaaminika kuwa ya kipindi cha mwanzo wa Uislamu na baadhi ya wataalamu kuihusisha na zama za Khalifa wa tatu, imehifadhiwa katika jumba la makumbusho lililoko msikiti wa kihistoria wa kijiji hicho. Nakala hiyo ina ukubwa wa sentimita 21 kwa 38 na imepambwa kwa alama za dhahabu, na inachukuliwa kuwa miongoni mwa nakala nne za Qur’ani zilizotumwa karne nyingi zilizopita kwa ajili ya kueneza Uislamu.

Kwa mujibu wa simulizi za wenyeji, nakala hiyo iligunduliwa takriban miaka elfu moja iliyopita na mchungaji aliyekumbana na sanduku la mbao alipokuwa akichimba karibu na mmea wa maua katika eneo la malisho. Eneo hilo baadaye likawa mahali pa heshima, na hatimaye msikiti ukajengwa, jambo lililopelekea kuanzishwa kwa kijiji cha Negel.

Mkutano wa Jumatatu uliwakutanisha wasomaji wa Qur’ani na wanaharakati wa Kikurdi kutoka maeneo mbalimbali ya Iran yenye wakazi wa Kikurdi, pamoja na washiriki kutoka Uturuki na Iraq.

Kongamano lilifunguliwa kwa kisomo cha kimataifa kutoka kwa Qari Vahid Nazariyan mwenye asili ya Kermanshah. Hujjatul Islam Karvand, mkuu wa Ofisi ya Waqfu na Masuala ya Hisani ya mkoa wa Kordestan na katibu wa mashindano ya kitaifa ya mwaka huu, alitoa hotuba ya makaribisho.

Hujjatul Islam Salehi, mkurugenzi wa Ofisi ya Waqfu ya mkoa wa Kermanshah, naye alihutubia washiriki. Ratiba iliendelea kwa visomo vya ziada na maonyesho kutoka kwa vikundi vya kaswida vilivyochaguliwa kutoka mashindano hayo.

Hadithi ya picha iliyochapishwa takriban miaka tisa iliyopita inaonesha Qur’ani hiyo ya kihistoria na msikiti unaoihifadhi.

3495089

captcha